Wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri aina ya PRO-BOX wilayani Bukombe wameondolewa hofu na kuaswa kuwa wavumilivu wakati wakisubiri majibu ya serikali kuhusu maombi yao kutaka kufanya safari zao nje ya mji kama ambavyo mabasi madogo na makubwa yamekuwa yakifanya jambo ambalo limekuwa ni changamoto kufuatia sheria kuwatambua kufanya huduma za teksi pekee.
Hayo yamejili Machi 13, 2023 wakati wa kikao cha mkuu wa mkoa Geita mhe.Martine Shigela na viongozi pamoja na wanachama wa umoja wa wamiliki na madereva wa PRO-BOX katika ukumbi wa Halmshauri ya Wilaya Bukombe huku akiwasisitiza kuwa watulivu na wenye kufuata sheria wakati suala lao linatafutiwa ufumbuzi.
Akiongea na kundi la vijana hao, Mhe.Shigela alieleza kuwa, lengo la serikali inayoongozwa na mhe.dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kutatua changamoto na migogoro inayowakabili wananchi ikiwemo waendesha PRO-BOX ambao wanaiomba serikali kuwaruhusu kufanya biashara tofauti na leseni zao zinavyowataka “kufanya kazi ya Teksi” ambapo amewaeleza kuwa, atatatua changamoto hiyo baada ya kuwasiliana na mamlaka ya juu inayosimamia sekta hiyo yaani Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na kisha kuwapa mrejesho wa maombi hayo.
“ni kweli mzunguko wa kukiodi Teksi kwa ushirombo bado ni mdogo, lakini kwa sasa niwaombe mzingatie, kwa wale wanaotaka kufanya Teksi endeleeni, lakini hekima mliyoiomba awali mkaruhusiwa kipindi cha nyuma, tunaweza kuomba tena itumike kwa kufuata utaratibu na kujiridhisha kulingana na mahitaji. Hivyo niombe muainishe uhalisia wa mahitaji yenu na kisha tutawasiliana na uongozi wa LATRA makao makuu ili tupate suluhu”
Vilevile mhe.Shigela amemaliza kwa kuwaambia kuwa, serikali hatikaki wananchi wake wawe masikini bali inataka wawe na mafanikio, hivyo suluhu itapatikana.
Naye kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoani Geita ACP Berthaneema Mlay amesisitiza juu ya uzingatiaji wa sheria kwa kundi hilo akionya tabia ya kujaza abiria kupita uwezo wa gari jambo ambalo huatarisha maisha yao.
Kwa upande wake Bw Rajabu Selemani ambaye ni Afisa mfawidhi kutoka LATRA alisema, “kwa mujibu wa kanuni namba 15 (h) ya leseni za usafirishaji (magari ya kukodi) “huduma zinazotolewa haziingiliani na huduma za daladala na gari za mji kwa mji” ambapo kwa hali hiyo wao wanatekeleza sheria ndiyo maana walizuia madereva hao kufanya safari nje ya eneo lao".
Mwenyekiti wa CCM (W) pamoja na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Bukombe kwa nyakati tofauti wamesema, wana imani kubwa na serikali inayoongozwa na mhe.rais dkt.Samia Suluhu Hassan kwamba italeta ufumbuzi wa changamoto hiyo.
Awali mwenyekiti wa umoja wa wamiliki na madereva wa PRO-BOX wilayani Bukombe bw.Anderson Antonio alisema wanaiomba serikali kutumia busara kuwaruhusu wafanye kazi kwa kubeba abiria na kwenda ruti za nje ya mji japokuwa ni kinyume cha sheria inayowasimamia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa