REDIO ZA JAMII ZAJENGEWA UWEZO KUHUSU MFUMO WA M-MAMA
Shirika la Pathfinder International limetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutoka katika Redio za kijamii zilizoko katika kanda ya ziwa ili waweze kutoa elimu kwa jamii zinazowazunguka kufahamu vyema mfumo wa m-mama na namna unavyofanya kazi.
Akifungua semina ya mafunzo kwa Redio za jamii kutoka mikoa ya kanda ya ziwa kwenye hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza Novemba 08, 2024 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amesema wanahabari kutoka kwenye Redio za kijamii wana nafasi kubwa ya kusaidia wananchi kuweza kufahamu mfumo huo ulioletwa mahsusi kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Dkt. Jesca Lebba ametoa wito kwa Redio za jamii kusaidia kuelimisha umma juu ya mfumo wa M-Mama unaotoa fursa ya usafiri wa dharula kwa Mama mjamzito, mama aliyejifungua ndani ya siku 42 na Mtoto mchanga mwenye umri usiozidi siku 28 kuanzia kwenye ngazi ya jamii hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ameongeza kuwa kulingana na tafiti zilizofanyika imeonekana kumekua na ucheleweshaji wa taarifa, miundombinu duni ya kufika kwenye vituo vya kutolea huduma pamoja na ucheleweshaji kwenye kupatiwa huduma mama wajawazito na watoto wachanga wanapofika hospitali hivyo mfumo huo umekuja na suluhisho kwenye adha hizo.
Akielezea kuhusu mradi huo, Mratibu wa mfumo wa M-Mama kutoka Mkoa wa Mara Stanley Kajuna amesema kuwa M-mama ni mfumo ulioanzishwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kama Vodacom Foundation, Pathfinder International, Touch Health kwa lengo la kuwawezesha mama mjamzito, mama aliyejifungua ndani ya siku 42, na mtoto mchanga hadi siku 28 kupata huduma za haraka anapopata dharura kwa kupiga simu namba 115 bila gharama yoyote.
Ndg. Kajuna ameongeza kwamba katika kuhakikisha usafiri wa dharura unaomsafirisha mlengwa bure mpaka kwenye kituo cha kutolea huduma za afya unapatikana kiurahisi jumla ya madereva jamii elfu nne wameshasajiliwa kwa ajili ya usafirishaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa