RUWASA YAPONGEZWA KWA KUTUMIA MFUMO WA NEST
Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Mbogwe imepongezwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 kwa kufuata taratibu za kutangaza zabuni za mradi wa maji katika Kata ya Ushirika Wilayani Mbogwe Mkoani Geita.
Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 Ndugu. Godfrey Eliakimu Mnzava amesema kuwa awali utaratibu uliokuwa unatumika kutangaza zabuni ulikuwa ni wa kubandika maombi na majibu ya waliopitishwa kutoa zabuni mbalimbali katika Taasisisi za Kiserikali, lakini Serikali ilibaini chembechembe za urasimu katika utaratibu huo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ameongeza kuwa baada ya Serikali kubaini changamoto katika utaratibu wa awali wa utangazaji zabuni ilihamisha utaratibu wa manunuzi na zabuni kuhamia katika mfumo wa kidijitali ambao umeweka uwazi na uwajibikaji unaotembea na mapinduzi ya sayansi na Teknolojia kwa sababu vigezo vyote vimeainishwa na waombaji watatambua kama wana sifa za kupata zabuni au la. Hivyo viongozi wote wa Mkoa wa Geita wahakikishe Taasisi zote za umma zitumie mfumo wa NEST kwa masuala yote ya kutangaza zabuni za utekelezaji wa miradi na manunuzi mbalimbali.
Ndg. Godfrey Mnzava pia ametoa pongezi kwa klabu ya kupinga rushwa katika Shule ya Sekondari Mbogwe kwa kuelewa vyema tatizo la rushwa linavyoharibu utaratibu katika matukio mbalimbali kama uchaguzi, nafasi za kazi, vyuoni na maeneo mengine na kutoa elimu kwa wananchi kupitia vibonzo walivyochora ambavyo vimetoa taswira nzima ya tatizo la rushwa.
Mradi wa Maji safi na salama katika Kata ya Ushirika ambao umegharimu Zaidi ya Shilingi Bilioni 2 utawanufaisha Zaidi ya wananchi elfu 20 wa vijiji vya Ushirika, Isebya, Ushetu, Mlale, Kadoke na Ikobe ambapo wananchi wa vijiji hivyo wametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo ambao utakuwa msaada mkubwa sana katika utatuzi wa changamoto ya uhaba wa maji.
Ukiwa wilayani Mbogwe Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 umeweka mawe ya msingi, kuzindua, kukagua na kutembelea miradi tisa ya maendeleo ambayo imegharimu shilingi Bilioni nne.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa