Na Boazi Mazigo-Geita
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kudhihirisha nia njema na upendo iliyo nao kwa kuwajali wananchi wake pale ambapo imeendelea kuridhia wananchi wa wilaya ya Bukombe kuendelea kufuga nyuki na kulina asali pamoja na mazao mengine ya nyuki kupitia mizinga ya nyuki waliyokuwa wameiweka kwenye Hifadhi ya Taifa Kigosi kabla ya kupandishwa hadhi kutoka pori la akiba Kigosi hapo awali.
Akiongea kwaniaba ya Serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii Agosti 24, 2022 siku ya pili tangu kuanza kwa zoezi la sensa ya watu na makazi, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Mary Masanja (Mb) amesema, serikali inayoongozwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan inatambua jitihada kubwa zinazofanywa na wananchi katika kujiletea maendeleo na ndiyo maana amefika kutatua changamoto iliyoibuka kutokana na kupandishwa hadhi pori la akiba kigosi na kuwa hifadhi ya taifa, hali iliyopelekea wananchi waliokuwa wanafanya shughuli za kujiletea kipato kupitia ufugaji wa nyuki kutakiwa kuondoka kwenye eneo hilo akisisitiza kuwa, serikali inatafuta mbadala wa maeneo hivyo waendelee kufanya shughuli hiyo kwa vibali kama ilivyokuwa awali mpaka pale watakapotatiwa maeneo hayo.
Mhe.Masanja amesema, “serikali inayoongozwa na Mhe.Rais Samia inatambua changamoto mnayopitia na ndiyo maana nipo hapa kwaniaba ya wizara. Niombe kwa sasa wananchi waliokuwa na mizinga yao kwenye eneo la hifadhi waendelee kufanya shughuli hiyo katika muda na kibali maalum na bila kuongeza eneo zaidi ya pale mizinga ilipokuwa wakati serikali inatafuta eneo mbadala. Vilevile, niwaombe tuwe sehemu ya uhifadhi na kutoa taarifa juu ya uharibifu wa mazingira ili kulinda misitu na kupata mahali pa kupata asali, kwani asali ni ajira”
“wananchi, kutokana na changamoto inayowakabili ya uharibifu wa mazingira, serikali pia inao mpango wa kuanzisha “Manzuki”, maeneo maalum ambayo yatatengwa na yatakuwa na mizinga siku zote, hakuna mtu ataweza kukata mti, ni kama nyumba ya nyuki maalum kwa ajili ya kuweka mizinga, hivyo muendelee kuwa na subira wakati tunaendelea kujipanga”. Ameongeza Mhe.Masanja.
Aidha, Mhe.Masanja amemaliza kwa kuwasihi wananchi hao kutokuuza bidhaa za asali kwa njia zisizo halali na kuwashauri kupeleka asali yao kwenye kiwanda cha serikali kilichopo mjini Ushirombo na kwamba huko watapata bei nzuri itakayowalinda, kauli ambayo ameitoa akiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Uyovu, kijiji cha Azimio wilayani Bukombe, kisha kuwakumbusha wananchi kushiriki kuhesabiwa kwa kutoa taarifa sahihi kwa makarani wa sensa na kuonesha nia ya kuifanya Bukombe kituo cha kujifunzia shughuli za uzalishaji mazao yatonakanayo na Nyuki ikiwemo maziwa ya Nyuki, Nta, Asali pamoja na sumu ya Nyuki.
Awali, Waziri wa Madini na mbunge wa jimbo la Bukombe Mhe.Dkt.Doto Biteko amesema, Mhe.Rais Samia anataka kuona kero za wananchi wakiwemo wa Uyovu zinatatuliwa na ndiyo maana Mhe.Naibu Waziri amefika, hivyo kuwasihi wananchi kuwa wahifadhi kwa kuilinda misitu ya Bukombe tena kwa wivu mkubwa ili isiharibiwe.
Naye RC Geita Mhe.Martin Shigela, ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi wa Uyovu kwa mapokezi mazuri akiupongeza uongozi mzima wa wilaya ya Bukombe kwa kuleta taswila ya maendeleo akisema, “Mhe.Rais Samia alinipa maelekezo kuja kushughulikia kero za wananchi, nitakuja. Niwaombe sana wataalam, dhana ya kusubiri mikutano ya viongozi isiwepo bali tangulieni mtoe majawabu kwa wananchi mapema kabla sijaanza ziara. Pia niwaombe mshiriki Sensa ya watu na makazi inayoendelea ili serikali iweze kupanga mipango yake".
Kwa upande mwingine wakiwa kwenye eneo la Matabe, Waziri wa Madini Mhe.Dkt.Doto Biteko (Mb), mkuu wa mkoa Geita Mhe.Martin Shigela, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja (Mb), Wakuu wa Wilaya za Bukombe na Chato pamoja na wakurugenzi wa Chato na Bukombe wameeleza juu ya wananchi wa eneo hilo kushiriki kuhesabiwa baada ya kuwa na utata juu ya mipaka ya maeneo ya wilaya mbili za chato na Bukombe na kuwaahidi kushughulikia suala hilo baada ya zoezi la sensa kukamilika.
Ifahamike kuwa, Wilaya ya Bukombe ina jumla ya vikundi vya wafuga nyuki 45 vyenye jumla ya wafuga nyuki 1,290. Vikundi hivi vina jumla ya mizinga 389,230 ya asili 369,018 na mizinga ya kisasa 6,297. Na, kwa kipindi cha miaka mitano (05) kuanzia mwaka 2017/2018 hadi mwaka 2021/2022 Wilaya ya ya Bukombe imesafirisha kilo 3,720,202 za Asali na kilo 243,124 za Nta ndani ya nchi na nchi jirani (Rwanda na Uganda). Aidha bei ya asali kwa kilo ni Sh. 3,600 na bei ya nta ni Sh. 8,000 kwa kilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa