Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema, serikali haitakubali bei elekezi kwenye zao la pamba ishuke hata kama changamoto zimejitokeza ili kuendelea kumuinua mkulima.
Amesema hayo julai 19, 2019 alipokutana na mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel akiwa ameambatana na wataalam wa wizara, bodi ya pamba na vyama vya ushirika walipofika ofisi ya mkuu wa mkoa wakati wa ziara yake mkoani hapa.
Akiongea baada ya kupokea taarifa ya sekta ya kilimo ya mkoa wa geita, Waziri hasunga ameeleza lengo la ziara yake mkoani hapa huku akiupongeza uongozi wa mkoa kwa usimamizi na kueleza msimamo wa serikali kuhusu bei ya pamba kwa mkulima pamoja na mipango ya serikali katika kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija
Amesema, “ziara hii inalenga kutoa ufafanuzi wa hali ya ununuzi wa zao la pamba ambapo jana nimekuwa na mikutano 8 Wilaya za Mbogwe, Bukombe na Geita. Niwapongeze kwa kuwa na uzalishaji wa chakula hadi kuwa na ziada ya tani zaidi ya 260,000 pamoja na hali ya mvua kusuasua”
Waziri Hasunga ameendelea kusema, changamoto ya ununuzi wa zao la pamba umetokana na kutikisika kwa soko la dunia, hivyo pamoja na hali hiyo bado msimamo wa serikali ni kwamba pamba inunuliwe kwa bei ya Tshs.1,200 kwa kilo na serikali itatoa dhamana kwa mabenki na wafanyabiashara ili waendelee kulipa kwa bei hiyo elekezi na ikitokea bei haijabadilika kukawa na hasara, basi serikali itaibeba ili wakulima wapate bei hiyo.
Amesema, “ipo haja ya kufufua viwanda vya nguo, kwani soko lipo, ni kufanya maamuzi ya dhati. Tuweke nguvu inayowekezana na wataalam watasaidia hilo”
Amesisitiza umuhimu wa mkoa kuongeza tija kwani kwa sasa uzalishaji upo chini kwa takwimu ya upatikanaji wa kilo hadi 300 kwa ekari 1, akitoa mfano wa nchi ya Israel kwa kuzalisha kilo 2,000 kwa ekari 1. Hivyo ameshauri jitihada ziongezwe ili mwakani angalau kuzalishwa kilo 1,000 kwa ekari, ili mkulima apate faida kwani mkulima anajilipa mshahara kwenye uuzaji mazao.
Amepongeza pia kilimo cha muwa wilayani geita na kusisitiza mpango wa serikali kwenye kuwezesha kilimo cha umwagiliaji, kwamba kwa sasa kutakuwa na maafisa umwagiliaji ngazi ya mkoa, na ngazi za halmashauri katika wilaya zote ambazo zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji ili maafisa umwagiliaji hawa wahahakikishe wanaanzisha na kusimamia skimu za umwagiliaji.
Amesema, kwa sasa nchi ina eneo la kilimo la hekta Mil 44 lakini linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta Mil 29.5 na linalotumika kwa kumwagiliwa ni Hekta 475,000 pamoja na kuwa na vyanzo vya maji.
Akamaliza kwa kusema, katika kupambambana na tatizo la viwavi jeshi pamoja na magonjwa ya mlipuko kwenye mazao, wizara inatarajia kuzindua bima ya mazao hivi karibuni ili kumkinga mkulima asipate hasara hivyo ni tegemeo la wizara kuwa kilimo kitachangia pato la taifa kwa kiasi kikubwa zaidi.
Awali mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel alitoa ombi la wizara kuboresha kilimo cha muwa na cha umwagiliaji kwa kupata timu ya watalaam watakaowezesha jambo hilo kufanikiwa.
Mathayo Maselle kwaniaba ya Katibu Tawala Mkoa aliwasilisha taarifa iliyoleza hali ya chakula na hali ya ununuzi wa zao la pamba iliyosema, mkoa ulilenga kulima hekta 657,442 kwa mazao ya chakula kwa lengo la kuzalisha tani 2,000,058 na hekta 98,334 za mazao ya biashara kwa lengo la kuzalisha tani 206,501. Hadi kufikia mwezi mei, 2019, jumla ya hekta 505,556 za mazao ya chakula sawa na 76.9% ya malengo zilikuwa zimelimwa na kuzalisha tani 1,332,184. Pia jumla ya hekta 102,182 za mazao ya biashara sawa na 103.9%
Kwa msimu wa ununuzi wa pamba uliofunguliwa mei, 2019 hadi kufikia mwezi julai 2019, ni tani 17,502.2 tu za pamba sawa na 34.7% ya pamba iliyozalishwa ndizo zimenunuliwa.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa