Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ameridhia shughuli za uchimbaji dhahabu kuendelea katika Mgodi wa Msasa Wilayani Bukombe baada ya kubaini idadi kubwa ya wachimbaji wadogo kutokuwa na mgogoro na mmiliki wa leseni.
Mhe. Shigela ametoa ridhaa hiyo tarehe 3 Februari 2026 katika kikao maalum cha wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Geita na Wilaya ya Bukombe pamoja na wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Msasa kilichofanyika katika Mji mdogo wa Runzewe Wilayani Bukombe.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amefafanua kuwa mmiliki wa leseni katika mgodi wa Msasa atachangia asilimia 50% za gharama ya uendeshaji akishirikiana na wachimbaji wadogo ambao pia watachangia asilimia 50 katika eneo la maduara yaliyopo ndani ya uzio.
Azimio hilo limekuja siku chache baada ya kuripotiwa kwa mgogoro uliotokana na utaratibu wa wa mgao wa asilimia 50 kwa 50 kati ya mmiliki wa leseni na wachimbaji wadogo mgodini hapo.
Mhe. Shigela amesema kuwa tathimini imebaini kuwa wamiliki wa maduara 273 yaliyopo ndani ya uzio sawa na asilimia 84 walishakubali kusaini mkataba wa mgawo wa asilimia 50. Hivyo kupitia tathimini hiyo utaratibu wa mgawo wa asilimia 50 utaendelea kama kawaida.
Azimio jingine lililotolewa na kamati ni agizo kwa maduara yote kuhakikisha maduara yote ya wachimbaji yaliyo kwenye hifadhi ya barabara mgodini hapo kuendelea kufungwa ili kulinda usalama wa barabara, hatua inayodhamiria kusimamia sheria ya ulinzi wa maeneo ya hifadhi ya barabara inayoagiza shughuli za uzalishaji kufanyika umbali wa mita 30 kutoka eneo la barabara.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita SACP Safia Jongo amesema jeshi la Polisi limejizatiti kuimarisha ulinzi na usalama katika mgodi huo huku akiahidi kufanyia kazi changamoto zote za kiusalama zitakazobainika.
Utatuzi wa mgogoro huo ni matunda ya vurugu zilizofanyika tarehe 22 Januari 2026 majira ya saa 3 asubuhi katika mgodi wa Msasa zilizohusisha wachimbaji wadogo Zaidi ya elfu moja na kupelekea shughuli za uchimbaji katika mgodi huo kusimamishwa pamoja na kufunga barabara kuu ya Kahama- kwenda Nchi jirani za Rwanda na Burundi kwa muda muda mfupi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa