Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Tshs. Bilioni 40 kwa ajili ya kujenga na kukarabati miradi tisa ya umwagiliaji inayotarajia kuwanufaisha zaidi ya wakulima elfu 40 wa mikoa ya Mwanza na Geita.
Mhe. Mtanda amebainisha hayo Agosti 08, 2025 alipokua akihutubia maelfu ya wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali katika kilele cha maadhimisho ya Nane nane Kanda ya ziwa magharibi yanayofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Pia ameeleza kuwa kwa kipindi cha 2020/25 serikali imetoa mbolea ya ruzuku ya Bilioni 6.4, Bilioni 4.7 kwa ajili ya ufugaji wa kisasa kwa vizimba ambapo zaidi ya vikundi 200 vimenufaika na Bilioni 263 zimetolewa kwa ajili ya chanjo za kuku na ng’ombe ndani ya mikoa hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ameziagiza Halmashauri kuendeleza viwanja hivyo kwa kuvijengea miundombinu ya kudumu na ya kisasa ili viwe na mazingira bora zaidi ya kuwahudumia wananchi katika kutoa elimu ya mashamba darasa kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa aliofanya kwenye sekta ya kilimo kwa kutuletea ruzuku ya pembejeo, kujenga maghala ya kutosha, kuwawezesha wavuvi kupata boti na nyavu pamoja na kuwapatia wafugaji madume yaliyoendelea kuboresha sekta ya mifugo.
Mhe. Shigela amewapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maonesho ya Nanenane ambayo ni fursa kwa wakulima na wafugaji kama sehemu ya biashara, maarifa kujifunza ili wanaporudi katika shughuli zenu za kilimo, ufugaji na uvuvi mkatumie maarifa mliyoyapata kuboresha na kuleta tija katika shughuli zao za uzalishaji.
Akitoa taarifa ya Maonesho hayo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Bw. Peter Kasele amesema wadau wameongezeka kutoka 1110 (2024) hadi 1234 (2025) ikiwa ni ishara ya wananchi kuhamasika kutaka kujua matumizi ya teknolojia katika kuongeza uzalishaji.
Kilele cha Maonesho hayo kimehitimishwa na utoaji tuzo na zawadi ambapo Aqwa Eagle (Magu) wameongoza katika uvuvi wa samaki, Fredrick Katundala (Nyamagana) ufugaji Nyuki, Mkulima bora akiwa ni ndugu Bulimi Zakaria (Kwimba) na Shija Mashauri (Nyang’hwale) akiibuka mshindi katika ufugaji bora wa ng’ombe wa nyama.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa