Yajayo yanaendelea kuushangaza mkoa wa geita na taifa la Tanzania kwa ujumla kufuatia mwendelezo wa ufunguzi wa masoko ya madini ya dhahabu mkoani hapa ambapo Agosti 05, 2019, Mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel amefungua soko la dhahabu wilayani Bukombe, linalofanya idadi ya masoko ya dhahabu mkoani Geita kufikia sita ikiwa mengine matatu yapo njiani kufunguliwa.
Akiongea na wananchi kabla ya uzinduzi wa soko hilo, mhandisi Gabriel ameeleza mafanikio ambayo mkoa umeyapata hadi sasa kwenye sekta ya madini, huku akisema bado kiu yake ni kuona lengo la sasa la ukusanyaji kwenye sekta ya madini linavuka mara nne zaidi, huku akiwapongeza wafanyabiashara wa dhahabu na kutoa maonyo mbalimbali juu ya utoroshwaji dhahabu pamoja na migogoro kwenye maeneo ya uchimbaji inayosababishwa na viongozi.
Amesema, “kama mkoa tumeona ya kushangaza baada ya uanzishwaji masoko ya dhahabu kwani hatukuwahi kupata hata kg.200 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo kwa mwaka huko nyuma ambapo mwaka 2018 mkoa ulipata kg.972.5 za dhahabu zenye thamani zaidi ya Bil 5.3, lakini kwa miezi sita ya mwaka 2019, tumepata kilo 1,160 za dhahabu, ambapo serikali imepata zaidi ya Bilioni 6 kama mrabaha, hivyo tuna uwezo wa kupata zaidi ya mara nne, tuna ongezeko la zaidi ya asilimia 200, haya ni mafanikio ya serikali ya awamu ya tano, ambapo kwa mwezi julai 2019 zimapatikana zaidi ya kg.300 za dhahabu”
Mhandisi Gabriel ameendelea kutoa wito kwa wafanyabiashara kuyatumia masoko ya madini huku akiwaagiza viongozi wa masoko ya dhahabu kupokea dhahabu kutoka kwa wafanyabiashara pasipo vikwazo vya mahali inapotoka na kuwaonya viongozi wanaosababisha migogoro kwa wachimbaji wadogo akikisisitiza kuwa haiupi mkoa heshima.
Mhandisi Gabriel amewashauri wafanyabiashara wa dhahabu kutumia mifumo ya kibenki kuepuka kubeba hela nyingi kwenye mifuko na kuwaagiza wakuu wa wilaya za mkoa wa geita kushughulikia migogoro ya wachimbaji na kuwaelekeza wananchi kutokujihusisha na imani potofu za kishirikina kwenye uchimbaji pamoja na wakati wa uchaguzi.
Mkuu wa wilaya ya Bukombe Said Nkumba amesema, katika kipindi cha Januari hadi Juni 2019, serikali imekusanya mrabaha kwa kiasi cha Tshs.400, 727,839 na ushuru wa huduma wa Tshs.1, 900,000 na halmashauri ya Wilaya ya Bukombe imefanikiwa kukusanya kiasi cha Tshs.302, 339,000 kama gawiwo la umiliki wa ardhi katika migodi iliyoko kwenye ardhi za halmshauri ya wilaya na serikali za vijiji.
Nkumba amesema, katika kutekeleza agizo la Mhe.Rais Magufuli la uanzishaji masoko ya madini, wilaya ya bukombe imeanzisha soko hilo la dhahabu katika jengo la serikali ambapo litasaidia kuboresha usimamizi wa mapato, kurahisisha utoaji wa huduma za serikali kwa wadau wa madini, kupata takwimu sahihi za uzalishaji wa dhahabu, kuimarisha usalama katika biashara ya madini ya dhahabu na kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini.
“Katika jitihada za kutatua changamoto ya ukosefu wa tafiti za kitaalamu kwa wachimbaji wadogo inayopelekea kuchimba kwa kubahatisha, kupitia wizara ya madini, serikali inajenga kituo cha mfano cha Katente kitakachowapatia wachimbaji wadogo utaalamu wa kuchimba na kuchenjua dhahabu” alisema Nkumba.
Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Geita Ernest Maganga amesema, wilaya ya Bukombe ina jumla ya leseni za utafiti 58, leseni za uchimbaji wa kati 1, leseni za uchimbaji mdogo wa madini 369, miradi ya uchenjuaji wa madini ya dhahabu 22, elution plants 2 na leseni ndogo za biashara ya madini 2 na kwamba mwaka 2017 yalifanyika marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ikiwa ni jitihada za serikali kudhibiti utoroshwaji wa madini nchini kwamba, kifungu cha 27C (1 na 2) cha Marekebisho ya Sheria ya Madini 2017 kinaelekeza uanzishwaji wa Masoko ya madini.
Wakati wa uzinduzi wa soko hilo, iliuzwa dhahabu yenye Gramu 23.0 ya Ubora wa 87% yenye thamani ya zaidi ya Tshs. 1,800,000
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa