Uwepo wa Chama cha Mawakala wa Pembejeo za Kilimo, Mifugo na Uvuvi Tanzania, Tanzania Agrodealers Association (TANADA) unatarajiwa kuleta mageuzi chanya kwa wauzaji wa pembejeo nchini kwa kuwawezesha kufanya biashara katika mtandao mpana, kuwa na mshikamano wa pamoja na kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni katika kikao cha pamoja cha kufufua chama hicho kilichowakutanisha wauzaji wa pembejeo za kilimo, mifugo na uvuvi kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Geita. Kikao hicho kilifanyika katika Mji mdogo wa Katoro, Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Akifungua kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Geita, Dkt. Elfas Msenya, amesema kuwa wauzaji wa pembejeo ni wadau muhimu katika mnyororo wa uzalishaji kwa kuwa wanawawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata huduma na bidhaa muhimu ikiwemo mbegu bora, mbolea, viuatilifu na pembejeo nyingine. Alisisitiza kuwa uwepo wa umoja imara unaowaunganisha ni jambo la msingi linalopaswa kupewa kipaumbele.
Dkt. Msenya alitoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuanzisha mchakato wa kufufua TANADA katika kila Mkoa, hatua inayolenga kuwawezesha wauzaji wa pembejeo kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo mikopo ya riba nafuu na programu za maendeleo.
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji aliwaasa wauzaji wa Pembejeo kuhakikisha wanafanya biashara katika mazingira rafiki kwa kuzingatia maduka yanakuwa na ukubwa na kuzingatia vipimo hitajika na kuruhusu hewa safi, pia wanasajili maduka yao na kutumia wataalam wenye vigezo kwenye maduka.
Aidha, aliwataka wauzaji wa pembejeo kushirikiana kikamilifu na wakulima, wafugaji na wavuvi kwa kuzingatia mifumo iliyowekwa na Serikali, akionya dhidi ya tabia ya kuuza pembejeo nje ya utaratibu rasmi pamoja na utoroshaji wa mbolea ya ruzuku, vitendo vinavyodhoofisha juhudi za Serikali na ustawi wa sekta hizo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mratibu wa Mradi wa Kuendeleza Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoka Wizara ya Kilimo, Bi. Justa Katunzi, amesema kuwa kupitia programu hiyo, upatikanaji wa mbegu bora na za kutosha utaongezeka na kuchochea uzalishaji wenye tija. Ameeleza imani yake kuwa wauzaji wa pembejeo Mkoa wa Geita watakuwa chachu ya kuimarisha umoja wao kwa kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji.
Mwenyekiti wa muda wa TANADA Mkoa wa Geita aliyechaguliwa ndani ya kikao hicho Ndg. Johnson Kilimokwanza, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwatambua wauzaji wa pembejeo kama wadau muhimu katika maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi. Amewahimiza wanachama wa TANADA kujitambua kama watu wa thamani, kushirikiana na Serikali, kutoa huduma bora kwa wateja wao na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya chama ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Ikumbukwe kuwa Umoja wa Wauzaji wa Pembejeo Tanzania ulianzishwa mwaka 2019 kupitia kikao cha kitaifa kilichofanyika katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali, umoja huo haukuweza kuendelea ipasavyo, hali iliyopelekea Serikali kuchukua hatua za makusudi za kuufufua ili kuimarisha sekta za kilimo, mifugo na uvuvi Nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa