Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela amepokea Tani 50 za mbegu ya alizeti kutoka Mamlaka ua Uthibiti wa Nafaka na mazao mchanganyiko ambazo zitagawiwa kwa wakulima katika Wilaya zote za Mkoa wa Geita.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mbegu hizo hivi karibuni katika viwanja vya GEDECO Geita Mjini Mhe. Shigela amesema Serikali inabadili sura ya wananchi wa Mkoa wa Geita kuacha kutegemea uzalishaji wa madini pekee na kuanza kuamini kwamba kilimo kinalipa pia.
“Tunabadili sura ya wananchi wa Geita sio tu kutegemea katika uzalishaji wa madini lakini pia wanaojishughulisha na kilimo watambue kuwa Serikali inafanya jitihada ya kuwawezesha ili waweze kufikia malengo ya kujiondoa kwenye umaskini.”
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba ameishukuru Serikali kwa kuwapatia wakulima tani 50 za mbegu ya alizeti kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uthibiti wa nafaka na mazao mchanganyiko Bi. Irine Makota amesema Mamlaka imetoa mtaalam ambaye atakuwepo Mkoani Geita kwa ajili ya kutoa elimu ya upandaji mpaka mavuno kwa wakulima watakaopata mbegu hizo. Pia kutakuwa na mnunuzi ambaye ataingia mkataba na wakulima wote watakaopata mbegu hizo kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na soko la uhakika la zao la alizeti kwa wakulima.
Mmoja wa wakulima waliopokea mbegu za alizeti, Marseli Maliganya mkazi wa kijiji cha Nyamboge Kata ya Shiloleli ameishukuru Serikali kwa kutoa mbegu hizo ambazo zitachochea uzalishaji wa zao la alizeti katika Mkoa wa Geita.
Marseli amesema kuwa huu ni msimu wa tatu tangu aanze kulima zao la alizeti na ameona kuwa ni zao lenye tija na lina nafasi kubwa katika harakati za kuwainua wananchi kiuchumi endapo wataendelea kupatiwa ushirikiano kutoka Serikalini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa