Ikiwa ni siku chache kuelekea Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa RCC, Wajumbe wa Bodi ya Barabara (RRB) Mkoa wa Geita wamezipongeza taasisi za Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS Mkoa wa GEITA na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini Tanzania TARURA Wilaya ya Geita kufuatia utekelezaji mzuri wa miradi ya ujenzi wa barabara wilayani Geita.
Pongezi hizo zimetolewa Januari 26, 2022 wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Geita walipotembelea miradi mitatu ya ujenzi wa barabara, mbili zikiwa za kiwango cha Changarawe na moja ikiwa ni ya kiwango cha Lami Nyepesi na kuipongeza halmashauri ya mji Geita wa ujenzi wa barabara ya lami kwa mapato ya ndani huku wakisisitiza uzingatiaji vipimo na viwango vya barabara ili kupata thamani ya miradi.
Kiongozi wa msafara wa wajumbe hao ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Mbogwe Mhe.Charles Kabeho amesema, wilaya ya Geita kwa ujumla imetekeleza vyema ujenzi wa barabara lakini pia ameishukuru serikali chini ya Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi kwani kwa ujenzi wa barabara hizo wananchi wataweza kufanya biashara wakisafirisha mazao yao lakini pia uwepo wa barabara hizo nzuri utasaidia shughuli za usafirishaji.
“kwanza tunaishukuru serikali kupitia Mhe.Rais kwa fedha zinazojenga barabara, vilevile tuwapongeze TANROADS na TARURA kwa barabara nzuri lakini pia TARURA niwaombe muhakikishe mkandarasi wa barabara ya Nyamikoma-Lwenge-Bugalama anafika mapema eneo la kazi kwaajili ya kumalizia kazi ndogo zilizobaki ikiwemo uwekaji alama kwenye daraja” alisema Mhe.Kabeho.
Wajumbe wengine walisisitiza juu ya halmashauri kukumbuka kujumuisha taa za barabarani kwenye mikataba ya ujenzi wa barabara za lami ili kuepuka kuchelewa kufunga taa za barabarani pamoja na uwekaji njia za waenda kwa miguu.
Kwa upande mwingine, wawakilishi wa taasisi za TANROADS na TARURA wamesema wataendelea kuzingatia ushauri uliotolewa na wajumbe hao ikiwemo ule wa kuboresha matengenezo kwenye barabara ya Nyankumbu-Nyang’hwale kupitia matengenezo maalum yaani Periodic Maintenance hata kabla ya lami kuanza kujengwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya usafiri na usafirishaji na kuepusha ajali na majanga mbalimbali yatokanayo na ubovu wa barabara.
Mwisho, wajumbe waliilekeza TANROADS Geita kufanya mawasiliano ya haraka na Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA juu ya muafaka ni Gati lipi litatumika eneo la Nkome ili lami ya km20 itakayoanza kujengwa, ijengwe na kuelekezwa katika eneo sahihi kama mipango inavyoonesha.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Nyamikoma-Lwenge-Bugalama yenye urefu wa Km.23 kwa kiwango cha Changarawe, matengenezo ya muda maalum Periodic Maintanance barabara ya Geita-Nzera Junction-Nkome yenye urefu wa Km.58 kwa kiwango cha Changarawe na mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mwanza Junction-Jengo la Utawala GTC-Hospitali ya Mkoa-Nyumba za Askari (Siro Barracks)-Chuo cha VETA yenye urefu wa Km1.3 kwa kiwango cha lami nyepesi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa