Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, TB, Madawa ya Kulevya na Magonjwa Yasiyoambukiza kwa pamoja wameiambia jamii ya Tanzania kupitia mkoa wa Geita kuwa, Tanzania bila maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI inawezekana kutokana jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania inayoongozwa na kiongozi shupavu Mhe.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo yameelezwa Mosi Machi, 2022 katika ukumbi wa Mwl.Julius Nyerere EPZ-Mjini Geita wakati wa kuahirisha kikao cha kamati hiyo baada ya kukutana na Konga la vijana na watu wazima wanaoishi na virusi vya UKIMWI ndani ya Halmashauri ya Mji Geita lililotanguliwa na ziara ya wajumbe wa kamati hiyo katika mkoa wa Geita kupitia Mgodi wa GGM, yenye lengo la kufatilia afua mbalimbali katika kupambana na magonjwa hayo, huku wakitoa shime kwa mkoa kuongeza juhudi katika mapambano ikiwemo kutafuta wadau wa sekta ya afya ili kwenda kwa kasi zaidi.
Akiongea wakati wa kuahirisha kikao hicho, mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe.Fatma Toufiq alisema, “ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita tunawapongeza kwa jitihada mnazozifanya kwa mfano Halmshauri ya Mji walivyotueleza kuokoa watoto wengi wanaozaliwa na wazazi wenye maambukizi ya VVU lakini wao wakatoka salama, hii inaonesha elimu inatolewa hongereni sana. Pia niwasihi, elimu hii iendelee na tuwatumie vijana wa rika sawa ili tuweze kufikisha ujumbe kwa wengi na kwa kufanya hivyo Tanzania bila UKIMWI inawezekana”
Mhe.Toufiq aliendelea kusema kuwa, “kipekee niwapongeze GGM, NACOPHA na TACAIDS kwa namna ambavyo nanyi mmekuwa msaada mkubwa kwenye mapambambano dhidi ya VVU. Nikifikiri jinsi leo ilivyo rahisi mtu kujisema waziwazi kuwa ameathirika ninaona jitihada ni kubwa hivyo niwaombe kazi iendelee".
Kwa upande mwingine Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Dkt.Sophia Mjema alisema, “kwanza niwakaribisheni sana Geita lakini mfahamu kuwa kama mkoa tumefarijika na ujio wenu, hatuna shaka nanyi ukizingatia mnafuatilia utekelezaji wa Ilani ya chama tawala CCM, hivyo tunaamini ujio wenu utaleta mabadiliko kwa wananchi kwakuwa nao wanaona fedha nyingi zinazotolewa na serikali yetu pendwa, hivyo karibuni sana”.
Naye Naibu Waziri wa Afya Mhe.Dkt.Godwin Mollel (Mb) alianza kwa kumpongeza Mganga Mkuu Mkoa wa Geita Dkt.Japhet Simeo pamoja na GGM akisema GGM ni ya Kuigwa na kuwaasa watumishi wa serikali kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuishauri kamati hiyo kuwa na pendekezo la kuwepo kamati itakayohusika na Sayansi na Uvumbuzi ili kuisaidia serikali na wananchi katika mazingira inapoibuka mijadala na hoja kuhusu wagonjwa wengi wa saratani kutoka kanda ya ziwa na sababu kuonekana ni shughuli za madini huku akiahidi kushughulikia changamoto zilizojitokeza zinazoikabili sekta ya afya.
Vilevile, Naibu Waziri wa Madini Mhe. Steven Kiruswa (Mb) alitoa pongezi za wizara kwa Mgodi wa GGM kwa kuwa wadau muhimu kwa serikali na kuahidi kushughulikia changamoto na ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa kuwa na siku maalumu ya kufanya kikao na mgodi ili kuja na majibu juu ya masuala mbalimbali yaliyoulizwa na wajumbe wa kamati.
Katika kuhitimisha, wajumbe mbalimbali akiwemo Mhe.Abdul-hafar Idrissa (Mb) alisema, ni muhimu kwa wabunge kuwa na kampeni ya wabunge vijana kuhamasisha zoezi la upimaji ili kuwahamasisha vijana wengine kupima afya zao na kujilinda lakini pia Mhe.Esther Malleko (Mb) akawapongeza NACOPHA na kuomba ziwepo jitihada za pamoja kulisaidia kundi la vijana kupitia mapambano dhidi ya VVU, TB na Madawa ya Kulevya na Magonjwa Yasiyoambukiza ili kuokoa nguvu kazi ya taifa.
Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima
Boazi Mazigo
Afisa Habari
Geita RS
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa