Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini TARURA Wilaya ya Geita wametakiwa kuhakikisha wanawasimamia ipasavyo wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya barabara wilayani humo ili kuleta tija na matokeo kwa wananchi na watumiaji wa miundombinu hiyo huku wakihakikisha miradi hiyo inazingatia vigezo na ubora uliyowekwa.
Hayo yameelezwa leo Machi 29, 2022 katika maeneo tofauti ya Jimbo la Busanda na la Geita wilayani Geita baada ya timu ya wataalam (wakiwemo wahandisi) kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita kufanya ziara ya ufuatiliaji wa miradi ya barabara inayotekelezwa na TARURA wilaya ya Geita.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Matengezo ya barabara ya Nyamikoma-Lwenge-Bugalama yenye urefu wa Km 14.5, ujenzi wa Boksi kalvati 1 na laini 7 za Kalvati, matengenezo ya barabara ya Bugalama-Idosero Km 8.5 pamoja na ujenzi wa Makalvati 6, zote zikiwa ni za kiwango cha changarawe kwa upande wa Jimbo la Geita kwa Jumla ya Tshs.492,579,540 na kwa upande wa jimbo la Busanda ni Matengezo ya Barabara ya Katoro-Nyabulolo-Nyalwanzaja yenye urefu wa Km 35 pamoja na ujenzi wa Boksi Kalvati 1 na Makalvati laini nane kwa gharama ya Tshs. 405,756,300
Akiongea akiwa eneo la miradi na wakati wa majumuisho Bw.Last Lingson ambaye ni Afisa kutoka idara ya Mipango na Uratibu ambayo inahusika na uratibu wa ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo amesema, ni muhimu kwa TARURA kuwa na usimamizi wa karibu sana wa miradi ya barabara hasa wakati wa utekelezaji ili kupata nafasi nzuri ya kutoa ushauri na maelekezo kwa wakandarasi kuliko kusubiri kukosoa baada ya utekelezaji.
“niwaombe TARURA, jitahidini sana kuwasimamia wakandarasi hasa wawapo saiti ili kuhakikisha wanazingatia masharti ya kazi na hata inapotokea changamoto iwe ni rahisi kuirekebisha mapema, kama ambavyo tumeona wakati tunazunguka, japo muda wa mkandarasi kukabidhi kazi haujaisha lakini unakaribia mwisho na bado kazi kubwa ipo kama kuweka udongo baada ya kuweka makalvati na kazi zinazoambatana na hiyo ikiwemo ushindiliaji”. Alisema Bw.Lingson.
Kwa upande wake Mhandisi Thereza Bernard kwaniaba ya Meneja TARURA wilaya ya Geita amesema, watahakikisha wanazingatia ushauri wote uliotolewa lengo likiwa ni kuwaletea watumiaji barabara huduma bora za usafiri na usafirishaji kwa maendeleo ya Geita na taifa kwa ujumla na kwamba watahakikisha pamoja na uhaba wa watumishi, wanaendelea kuomba watumishi wengine ili kuongeza nguvu kazi na kutumia rasilimali chache walizonazo kwa sasa kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi hata kama kuna upungufu.
Miradi yote miwili iliyotembelewa ina gharama ya Tshs.897, 615,840 ambapo hadi sasa miradi hiyo yote imetekelezwa kwa wastani wa 90% na kuendelea.
Ziara hii, itaendelea kwenye Wilaya za Nyang’hwale, Bukombe na Chato.
Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima. Kazi Iendelee.
Boazi Mazigo
Afisa Habari
Geita - RS
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa