Inakadiriwa kuwa zaidi ya wananchi wapatao elfu kumi (10,000) wanatarajiwa kunufaika baada ya ukamilishwaji wa Boksi kalvati (daraja) linaloendelea kujengwa kwenye Mto Iyenze katika mradi wa barabara ya Mwingiro-Ng’wasabuka katika Kata ya Mwingiro wilayani Nyang’hwale, daraja litakalowaunganisha wananchi wa vijiji vya kata ya Mwingiro ikiwemo vijiji vya Mwingiro, Iyenze na wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala iliyopo mkoani Shinyanga wilaya ya Kahama litakalogharimu kiasi cha Tshs.119, 000,000.
Hayo yameelezwa na wataalam wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini TARURA Wilaya ya Nyang’hwale Machi 30, 2022 wakati wa ziara ya timu ya wataalam kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita ambao wanaendelea kufanya ufuatiliaji wa miradi ya barabara inayotekelezwa na TARURA kwa mwaka wa fedha 2021/2022, ambapo kwa Nyang’hwale walipita kwenye miradi 6 yenye jumla ya Tshs. 545,731,000 zinazotokana na fedha za Tozo ya mafuta.
Akiongea akiwa kwenye maeneo mbalimbali ya miradi na wakati wa majumuisho, Bw.Last Lingson ambaye ni Afisa kutoka idara ya Mipango na Uratibu ambayo inahusika na uratibu wa ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo akiwa na wataalam wengine wa ofisi ya mkuu wa mkoa aliwapongeza TARURA Nyang’hwale kwa namna wanavyoendelea kutekeleza majukumu yao kwenye usimamizi wa miradi mbalimbali ya barabara huku akiendelea kusisitiza juu ya usimamizi wa karibu zaidi kwa wakandarasi wanapoelekea kumaliza kazi, lengo likiwa ni kuleta matokeo kusudiwa.
“tuwapongeze TARURA Nyang’hwale kwa kuwa mmejenga barabara zenu vizuri, na mtakapokamilisha daraja lile kwenye Mto Iyenze na barabara ile ya Bukwimba-Bulangale kwa hakika mtakuwa mmewasaidia wananchi wengi kwani kwa kufungua barabara ambayo haikuwepo na kwa kuwaunganisha wananchi wa pande hizi za Mwingiro na Ng’wasabuka ni dhahiri mtachochea maendeleo kupitia sekta ya usafiri na usafirishaji” alisema Bw.Lingson.
Vilevile Bw.Lingson aliwakumbusha kuendelea kuhakikisha ushauri wote uliotolewa na wahandisi uzingatiwe ili kwa pamoja kufanikisha azma ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara.
Kwa upande wake Mhandisi Elson Moshi kutoka TARURA Nyang’hwale alisema, wao wamejipanga kuendelea kuwasimamia wakandarasi wote wanaotekeleza miradi kwenye wilaya yao na kuhakikisha wanatekeleza masharti ya mkataba lakini kubwa zaidi kutoa matokeo tarajiwa kwani japokuwa kazi hazijakamilika lakini tayari wanapata mrejesho kutoka kwa wananchi kuwa kazi wanayoifanya ni njema na inawasaidia wananchi, wakiahidi kuzingatia ushauri uliotolewa na wataalam ngazi ya mkoa. Mhandisi Moshi alieleza pia changamoto ya wakulima wanaolima karibu kabisa na miundombinu ya barabara pamoja na ile ya mifugo kupita kwenye barabara zilizotengenezwa ambazo hupekelea uharibifu mkubwa.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na matengenezo ya sehemu korofi katika barabara za Mang’ombe urefu wa Km.3.0, Nyashilanga-Nyamigogo urefu wa Km.3.0, Ujenzi wa Boksi Kalvati 1 katika barabara ya Mwingiro-Ng’wasabuka. Vilevile Matengenezo ya sehemu korofi katika barabara za Busolwa-Gamashi Km.11.4 na Nyamishishi-Shibalanga-Kaboha yenye urefu wa Km.7.0, na Ukarabati katiba barabara ya Bukwimba-Bulangale yenye urefu wa Km.5.0.
Pamoja na mvua zinazoendelea kunyesha, bado miundombinu hii inaendelea kustahimili na kuonekana iko vizuri na kwa hakika, kazi inaendelea.
Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima. Kazi Iendelee
Boazi Mazigo,
Afisa Habari
Geita RS
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa