Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amefanya ziara kutembelea na kujionea hatua ya ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa geita katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa Hospitali za Rufaa za mikoa nchini julai 17, 2019
Wakati wa maelekezo ulipowadia, Waziri Ummy akamtaka mkandarasi ambaye ni wakala wa majengo nchini TBA kukamilisha ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo lengo likiwa ni kuanza kutoa huduma tarehe 1 desemba, 2019.
“mkandarasi nakuagiza kufanya kazi kwa bidii, nikabidhiwe majengo haya tarehe 30 mwezi oktoba kwakuwa ni lazima huduma zianze kutolewa mwezi desemba mwaka huu kwani serikali kupitia Mhe. Rais Magufuli imetoa Bilioni 2.56 kwaajili ya ukamilishaji wa kazi hii, hivyo hakuna sababu ya kuchelewa bila kusahau matumizi ya nguvu kazi (force account)”, alisema Waziri Ummy
Waziri Ummy amewaeleza viongozi aliokuwa pamoja nao kwenye ziara hiyo akisema kuwa wanapaswa kutambua hiyo ni hospitali ya mkoa wa geita, hivyo ni vyema kuunganisha nguvu kwa pamoja kuhakikisha inakamilika.
Uongozi wa Mkoa vilevile umepongezwa kwa namna ulivyojitahidi kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 80 mwezi juni 2018 hadi vifo 31 mwezi juni 2019 huku kukiwa hakuna magonjwa ya mlipuko kwa mwaka mzima.
Waziri Ummy amezitaka halmashauri pia kujipanga kuajiri vijana walio tayari kujitolea kwa kuwalipa kiasi fulani cha kujikimu kupitia mapato ya ndani, vijana ambao endapo nafasi za ajira zitatoka watapewa kipaumbele wakati serikali pia ikiendelea kuajiri kwani haiwezi kutosheleza mahitaji yote kwa wakati mmoja huku akitoa rai kwa vijana waliomaliza fani ya uuguzi kuwa tayari kujitolea kufanya kazi hizo.
Akimaliza, waziri ummy amemshukuru mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Gabriel pamoja na wataalam kwa usimamizi mzuri wa sekta ya afya mkoani geita ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya afya vilevile kushukuru kwa kupata kibali kutoka kwa katibu mkuu utumishi cha kuajiri watumishi wa afya hivyo kuahidi baadhi ya watumishi kupelekwa mkoani geita.
Majengo yanayotajwa kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo ni pamoja na wodi ya wazazi, Maabara na wodi za wagonjwa.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel amesema, kukamilika kwa ujenzi wa majengo hayo yaliyobaki kutaleta maana halisi ya kuwa na hospitali hiyo akisema’ “Uwepo wa wodi ndio utatoa taswira ya kuwa Hospitali hii kuwa ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, ili mtu akipata Rufaa aweze kulazwa na kuchukuliwa vipimo" .
Nao Wahe. Wabunge Lolesia Bukwimba na Vicky Kamata wamemshukuru waziri ummy kwa kuendelea kuitendea haki wizara ya afya kuboresha maisha ya wananchi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa