Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela, amesema kuwa programu ya Mradi wa Thamini Uhai utaleta tija na kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Mhe. Shigela ameyasema hayo tarehe 12 Februari 2026 alipokuwa akizindua rasmi mradi huo katika Ukumbi wa mikutano Otonde uliopo Geita mjini.
Mkuu wa Mkoa amebainisha kuwa uwepo wa mradi huo utaongeza vifaa, kuongeza watumishi katika maeneo yenye uhaba wa wafanyakazi, kuongeza uhamasishaji kwa jamii, pamoja na kuimarisha miundombinu ya vituo vya afya ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto kabla, wakati na baada ya kujifungua.
Mhe. Shigela ametoa shukrani za dhati kwa Shirika la Thamini Uhai kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo wanazidi kutoa mkazo na kuunga mkono jitihada za Mkoa wa Geita katika kuhakikisha inaboresha masuala ya afya ya uzazi na kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Mwakilishi kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bi. Jesca Tryphone amewaasa wataalam wa Afya katika maeneo yote ambayo mradi utatekelezwa waendelee kuimarisha uwajibikaji katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kusimamia vyema mfumo wa mapato na matumizi katika vituo vyao kwa lengo la kupata mapato yatakayowawezesha kununua dawa na vitendea kazi vingine.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mradi wa Thamini Uhai Banzi Msumi, amesema lengo la mradi huu ni kuunga juhudi za Serikali katika kupunguza vifo vya mama na mtoto mchanga,kuboresha huduma za dharura za uzazi na mtoto mchanga, huduma bora za kliniki za wajawazito na ufuatiliaji,kupanua upatikanaji wa kinga na tiba kwa watoto na akina mama baada ya kujifungua,kutoa ushauri wa kitaalam,utafiti na ufuatiliaji wa takwimu kwa Kushirikiana na Wizara ya Afya.
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Geita,Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Mhe.Mhandisi Paskasi Muragili ameahidi kuwa mradi wa Thamini Uhai utapewa ushirikiano thabiti na kuhakikisha Mkoa wa Geita unakuwa wa kwanza katika utekelezaji wa kupunguza kabisa vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Mradi wa Thamini Uhai utatekelezwa katika vituo 160 vya Afya ndani ya Mikoa ya Geita, Kigoma na Katavi katika kipindi cha miaka mitano kuanzia Novemba 2025 hadi Juni 2030 kwa gharama za Dola za Kimarekani Milioni 12 ambapo Mikakati ya Mradi huo ni pamoja na Kuboresha huduma za dharura za uzazi na mtoto mchanga, huduma bora za kliniki za wajawazito na ufuatiliaji, kupanua upatikanaji wa kinga tiba kwa watoto na akina mama baada ya kujifungua na ushauri wa kitaalam, utafiti na ufuatiliaji wa takwimu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa