Mkuu wa mkoa wa Geita mhe.Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuacha kuvamia misitu ili kulinda mazingira kwa maisha endelevu.
Mhe.Senyamule ameyasema hayo Februari 11 na 12,2022 alipofanya ziara kwenye hifadhi za misitu iliyopo wilayani Geita akiwa ameambatana na maofisa wa Wakala wa Misitu Tanzania TFS kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhifadhi wa mazingira, akipanda mti kwenye eneo la msitu wa Geita kama ishara ya uzinduzi wa kampeni ya uhifadhi wa mazingira na kuwataka wananchi kuacha kuvamia na kujimilikisha maeneo ya hifadhi ili kuwa na jamii endelevu.
“tunamshukuru mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kata ya Lwamgasa nayo imepokea fedha za madarasa mengi kwenye mkoa pamoja na miradi mingine. Tumedhamiria kurudisha uhai wa mkoa kupitia uhifadhi, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuwa mlinzi wa mwingine hasa baada ya mavuno ili baadaye tupande miti ili tutunze mazingira ikiwemo vyanzo vya maji. Vilevile niwahakikishie wananchi juu ya upatikanaji wa umeme kwenye vijiji 124 vilivyosalia kwani tayari serikali imetuletea mkandarasi mpya CSJE-CTCE Constrium kwaajili ya utekelezaji mradi wa REA III mzunguko wa pili kwa gharama ya Bilioni 25.4”, alisema mhe.Senyamule.
Wakati akimaliza kuongea na wananchi, mhe.Senyamule aliwakumbusha wananchi hao juu ya kujiandaa na sensa ya watu na makazi na kuwahimiza kushiriki na kutoa taarifa sahihi wakati zoezi litakapoanza.
Kwa upande wake Mhifadhi wa Misitu Wilaya ya Geita Almas Mggalu amesema, misitu ya Geita imeharibiwa kwa kiasi kikubwa na ndiyo maana wanakuja na mpango wa kuanzisha misitu ya kupanda kutokana na kuharibiwa ile ya asili na kuwataka wananchi kuendelea kuzingatia sheria iliyopo inayolinda hifadhi za misitu kwa manufaa yao ya sasa na ya baadae.
Aidha, wananchi wa Samina, Kata ya Mtakuja iliyopo halmashauri ya mji Geita na wa Lwamgasa ndani ya halmashauri ya wilaya ya Geita wameendelea kuiomba serikali kuwapatia maeneo zaidi kwa ajili ya kilimo na ufugaji kufuatia maeneo yao kuzungukwa na mgodi pamoja na hifadhi za misitu ambapo awali mhe.Senyamule aliwaeleza kuwa, ni vyema kuendelea kusubiri tume iliyoundwa itakapoleta majibu juu ya maombi yao ya ardhi.
Katika ziara hiyo, mhe.Senyamule alisikiliza na kuelekeza utatuzi wa kero na changamoto mbalimbali zilizoibuliwa na wananchi wa maeneo hayo ili ziweze kushughulikiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa