Na Boazi Mazigo - Geita
Wananchi na wakazi wa Kata ya Muganza Wilaya ya Chato Mkoani Geita wameiangukia serikali na kuiomba radhi kufuatia tukio la kubomoa na kukichoma moto kituo cha polisi Muganza, tukio walilolitekeleza Machi 30, 2023 kwa madai ya kutoridhishwa na sababu za kifo cha mtuhumiwa wa wizi wa betri Enos Misalaba (32) ambaye kwa sasa ni marehemu ambaye ilielezwa alifariki kutokana na kuumwa lakini wao wakidai alifariki kutokana na kupigwa na askari polisi.
Hayo yamejili Aprili 7, 2023 wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.Mhandisi Hamad Masauni katika kata ya Muganza-Chato ambaye alieleza kusikitishwa kwake kwa kitendo kilichofanyanyika na kutoa onyo kwa wananchi kujichukulia sheria mkononi akiwasihi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kudumisha amani na usalama kwa kuzingatia uwekezaji mkubwa uliopo na unaoendelea.
“kwakuwa serikali inayoongozwa na Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa sana kwa maendeleo ya watu ninyi ni mashahidi, imani yangu kuwa nyie ndio kuisaidia serikali katika kuhakikisha mnaimarisha ulinzi katika maeneo yenu, lakini msipotoa ushirikiano kwa jeshi la polisi mnaweka rehani usalama wenu. Ilinishangaza sana watu ambao hawalali kuhakikisha mnaishi salama, nyie mnakua mstari wa mbele kuhujumu rasilimali za jeshi la polisi, hili halikubaliki hata kidogo na sitarajii kuona tena suala hili baada ya ninyi kuomba radhi”, alisema Mhe.Masauni.
Mhe.Masauni aliongeza kuwa, wapo viongozi wanaowakingia kifua wahalifu kwa misingi ya kuwa ni wanachama wao, hivyo kusema inapotokea uhalifu, sheria huchukua mkondo wake kwa yeyote atakayefanya mambo kinyume na utaratibu na kusisitiza kuwa kauli kama hizo huvuruga umoja na mshikamano ambao umejengwa na Mhe.Rais Dkt.Samia.
Alimaliza kwa kuipongeza CCM kutoa jengo lake na kulifanya kituo kwa muda, kisha kupongeza juhudi za mkoa na wilaya kwa jitihada wanazozifanya kuimarisha ulinzi na kuwataka walioanza kuchangia ujenzi waendelee na wito kutolewa kwa jeshi la polisi na wote wanasimamia usalama wa wananchi kutekeleza majukumu yao kwa misingi ya sheria na ikiwa kuna askari anaenenda kinyume basi ashughulikiwe na ngazi ya wilaya na mkoa
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Geita Mhe.Martine Shigela aliwakumbusha wananchi kufuata hatua mbalimbali kwa kuwaona vingozi na kuwasilisha kero zao katika kutatua changamoto kuliko kujichukulia sheria mkononi
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa Geita ACP Safia Jongo alisema yeye havumilii vitendo ambavyo si vya kiuadilifu na kuwasihi kufuata taratibu na kwamba kitendo kilichofanyika siyo cha kiutu wala si cha kibinadamu. Hivyo kuchukua nafasi hiyo kukemea na kuwataka wananchi kuheshimu dola na kuwaahidi haki kutendeka kwa waliohusika.
Awali wananchi hao walipewa nafasi ya kuongea ambapo waliwakilishwa na Bw.Dismas Joshua na Bi.Mary Josephat ambao waliomba radhi kwa serikali kufuatia tukio hilo na kuahidi kutojirudia wakisisitiza kuwa kata yao ni kubwa na ina biashara nyingi hivyo upo umuhimu mkubwa kuwa na kitio cha polisi.
Geita Bila Sheria Mkononi Inawezekana
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa