Ikiwa ni siku moja baada ya kufanyika Jukwaa la Fursa za Biashara Mkoani Geita, kampuni ya kuuza magari makubwa, vipuri na mitambo ya GF-Trucks & Equipment imefungua duka lake la vipuri vya magari,na uuzaji magari Tarehe 18.08.2018 katika Kata ya Buharahara Mtaa wa Magogo Mjini Geita.
Akizungumza kabla ya kufungua duka hilo ambalo pia litakuwa likuza magari, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amesema, uwekezaji huo ni moja ya matunda yatokanayo na jukwaa hilo hivyo wawekezaji hao hawatajuta kwakuwa wamechagua sehemu sahihi kuwekeza.
“Napenda kuwashukuru sana uongozi wa Magazeti ya Serikali kwa kushirikiana nasi kuandaa jukwaa hilo lililoanza kuzaa matunda. Wateja wengi walikuwa wanasononeka mko mbali na kufanya vipuli kutopatikana kwa urahisi, ila kwa ujio wenu huu hakika nawapa pongezi nyingi.
Pia niwape pongezi uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa mipango mzuri wa mji. Atoa wito kwa wananchi kuwa, Kuna sababu kubwa ya kutumia vifaa na mitambo ya GF Truck & Equipment kwa kuwa, unapata matengenezo mwaka mmoja bure” wachimbaji waje wachukue mitambo. Amesisitiza kuwa kwa sasa mwananchi haitaji kupanda ndege bali apande hata boda boda kufika Haga Auto Garage kujipatia magari mapya na ya kisasa kwa shughuli mbalimbali hasa za madini.
Amekaribisha uwekezaji kiwanda cha magari lakini pia akatumia fursa hiyo kuiomba kampuni hiyo kusaidia upande wa michezo kwa kudhamini timu za Mkoa wa Geita. Kipekee Mhe. Mhandisi Gabriel akatoa tahadhari kwa kampuni ya Haga Auto Garage kuwa kama ameaminiwa na mwekezaji bali asimwangushe kwa kuhakikisha bei ya vipuli haizidishwi jambo ambalo laweza fukuza wateja na kupunguza uaminifu. Hivyo Mkuu wa Mkoa ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kwani Geita haina urasimu lakini pia awashauri Gf Trucks kuwatumia walimbwende wa mkoa kutangaza biashara yao.
Mbunge wa jimbo la Geita Mjini Mhe. Constantine Kanyasu akamshukuru mwekezaji GF Truck & Equipment kwa kuichungulia fursa na kumpongeza wakala wa mitambo hiyo Haga Auto Garage na kusema yeye kama mwakilishi wa wananchi wakiwemo wao wafanya biashara ataendelea kuwatetea.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Josephat Maganga akawapongeza GF Truck & Equipment kwa kufanya yale ambayo serikali ya mkoa inayataka ya kutanua uwekezaji na kuipongeza Haga Auto Garage kwa kuwa mwenyeji mzuri kumpokea mgeni mwekezaji na kushauri waweke magari ya kutosha wananchi waelewe kuwa wao ni wauzaji wakubwa wa magari.
Mkurugenzi wa Mji Geita Mhandisi Modest Apolinary akawashukuru na kuwakaribisha pia katika shughuli za miradi ya jamii kama ujenzi wa mashule, zanati n.k
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhe. Leonard Bugomola pamoja na mwenyekiti wa TTCIA ndugu Chacha Wambura Mkoa wa Geita wakapongeza matunda ya jukwaa la fursa na kuwashawishi wananchi wa Geita wasiende mbali kununua magari ya kazi bali waende Haga Auto Galage wapate magari ya kampuni ya GF Trucks. Pia ndugu Wambura akatoa hitaji lake la kuhitaji magari mawili kutoka kwao na kusisitiza kuwa ni vyema huduma zote za kampuni hiyo zipatikane Geita na siyo Dar es Salaam yalipo makao makuu ya ofisi za GF Trucks
Mkurugenzi Mtendaji wa GF Truck & Equipment ndugu. Alijawad Karmali amesema “nashukuru kukaribishwa mkoani Geita na nimeshuhudia kuwa Mkuu wa Mkoa ni mtu wa kazi, hivyo nakupongeza Mhe. Mkuu wa Mkoa na ninaahidi kufanya kazi nzuri nanyi”, akamaliza.
Afisa Masoko wa GF Truck & Equipment ndugu Kulwa Bundara akasema moja ya sababu iliyowafanya wawekeze mkoani Geita ni amani iliyopo lakini pia kuondoa shida ya vipuli feki kutoka kampuni hiyo ambavyo vimekuwa vikuzwa na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Mkurugenzi wa Haga Auto Garage, ndugu Ali Gandi akamhakikishia Mkuu wa Mkoa kufanya kazi kwa uaminifu lakini pia kuhakikisha anawasimamia watumishi waliyo chini yake kuhakikisha wanazingatia misingi.
Miss Geita Bi. Joyce Magesa na mwenzake Mshindi namba mbili bi. Angel David wakatumia fursa hiyo kusema kuwa wapo tayari kuitangaza kampuni hiyo na kuomba kampuni hiyo kuwa tayari kuwaoa ushrikiano katika jukumu la kijamii wanalotarajia kulifanya ndani ya mkoa la kuelimisha wanafunzi na kuwahamasisha kuepuka vishawishi ili waweze kusoma na kumaliza masomo yao.
Mwisho mgeni rasmi akazindua uuzaji wa magari makubwa (matipa) kwa kuwasha gari, pamoja na ofisi ya kuuzia vipuli vya magari hayo kisha kukabidhi hati ya uwakala kwa Kampuni ya Haga Auto Galage.
Hafla hiyo fupi pia ikahudhuriwa na Katibu Tawala Wilaya ya Geita, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita, Diwani wa Kata ya Buhalahala, na Kaimu Afisa Tarafa ya Geita Mjini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa