Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Rosemary Senyamule amesema, ni muhimu kwa Kamati kuhakikisha maelekezo yote juu ya utoaji wa chanjo ya Polio yanazingatiwa ili kutekeleza maagizo ya serikali kuhakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano (5) wanapata chanjo hiyo ili kulikinga taifa, huku akisisitiza kila mjumbe kuwa balozi wa chanjo hiyo na kukemea wapotoshaji na kuwaelimsha wenye imani potofu.
Hayo yameelezwa Aprili 22,2022 na mkuu wa mkoa wa Geita wakati akifungua kikao cha kampeni ya Chanjo ya Polio kwa Kamati ya Afya Msingi (PHC) katika ukumbi mdogo wa ofisi ya mkuu wa mkoa kisha kutoa tahadhari kwa wale wote watakaojitokeza na propaganda za uongo kwa lengo la kupotosha lengo la serikali la kuwakinga wananchi wake huku akitoa pongezi nyingi kwa serikali kwa kujali afya za wananchi wake.
Mhe.Senyamule alisema, “kwanza tuishukuru serikali yetu chini ya Rais wetu mpendwa Mhe.Samia Suluhu Hassan kupitia wizara ya afya kwa namna anavyoendelea kuwajali wananchi hata kupitia utolewaji wa chanjo hii. Lakini pia niwaombe, kwakuwa serikali imechukua tahadhari kwa haraka baada ya kutokea mlipuko kwenye nchi jirani, basi sisi tukawe mabalozi kuhamasisha kila mzazi kuhakikisha mtoto mwenye umri chini ya miaka 5 anapata chanjo hii”
Vilevile, Mhe.Senyamule aliwataka wajumbe kuhakikisha wanakemea propaganda potofu ambazo huwa zinajitokeza wakati zinapoletwa chanjo akisema, “ni muhimu sana kukemea uongo utakapoibuka kwenye zoezi hili kwani Uongo Usipokemewa Utahesabika kuwa Ukweli”
Akihitimisha, Mhe.Senyamule alisema uwazi ni jambo pekee litakalosaidia kuongeza ufanisi hususani kwa mambo yasiyo ya usiri lakini pia akatumia wasaa huo kuhimiza viongozi kuendelea kuwahamasisha wananchi kujiandaa kushiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi pale itakapoanza Agosti, 2022
Naye Mganga Mkuu Mkoa Dkt.Japhet Simeo alisema, ni muda mrefu tangu mwaka 1996 Tanzania kupata ugonjwa huu na pia kutakuwa na zoezi la kuwatafuta na kuwafatilia watoto wote wenye umri chini ya miaka 15 ambao wamepata ulemavu wa ghafla tepetepe (washukiwa wa ugonjwa wa Polio) na kutoa taarifa katika vituo vya karibu kwa uchunguzi na kubaini ugonjwa huu wa Polio
Kwa upande mwingine, Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa Ndg. Wille Luhangija alisema, zoezi la chanjo litahusisha mkoa mzima na linatarajiwa kuwafikia takribani watoto 553,228 wa umri chini ya miaka 5 na litaanza kuanzia tarehe 28.04.2022 hadi tarehe 1.05.2022.Ndg. Luhangija alisema kuwa, kutakuwa na timu ya wataalam watatu mmoja akiwa ni mchanjaji, mwingine mtunza kumbukumbu na mwingine mhamasishaji na watahakikisha zoezi hilo linaenda vizuri.
Geita ya Dhahabu Utajiri na Heshima, Kazi Iendelee
Boazi Mazigo
Ag.HGCU
GEITA RS
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa