Na Boazi Mazigo- Geita
Hadi hivi leo Agosti 12, 2022 zikiwa zimebaki siku 11 kuelekea Sensa ya Watu na Makazi, Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.Martin Shigela amefungua kikao kazi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA cha kupitia malengo ya robo ya kwanza mwaka wa fedha 2022/23 kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu na Mara katika Ukumbi wa Mikutano uliopo jengo la Otonde Mjini Geita msisitizo mkuu ukiwa ni kuhakikisha walipa kodi wanatoa risiti za mfumo EFD wanapouza huduma au bidhaa.
Akizungumza na washiriki wa kikao hicho ambao ni maafisa wa TRA, RC Shigela amewapongeza TRA Kanda ya Ziwa kwa kufikisha zaidi ya asilimia 100 ya lengo walilopangiwa na kutoa onyo kwa wafanyabiashara ambao wanashiriki kuipotezea serikali mapato kwa kutotoa risiti akisema ni kupitia kodi hizo wananchi ndipo hupata huduma za maji, elimu, afya, mishahara kwa watumishi n.k
Wakati huo huo, RC Shigela ametoa rai kwa wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa au huduma na kwamba hata ongezeko la mishahara na upandaji madaraja watumishi ni kunatokana na wananchi kuisaidia serikali kwenye eneo hilo kwani unapopewa risiti ya EFD ndipo serikali inapata mapato stahiki
"ninatambua kazi nzuri mnayoifanya TRA, nawaahidi ushirikiano kama kiongozi wa mkoa huu, na niwaombe tujipange kukusanya zaidi ya asilimia 100 ya lengo letu kwa mwaka huu, tutumie fursa aliyoitengeneza Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwafanya Wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari bila hata kutumia nguvu ambapo tumeshuhudia ndani ya mwaka mmoja wa Mhe.Rais, mapato yameongezeka kwa kiasi kikubwa". Amemaliza RC Shigela kisha kufungua kikao hicho cha siku mbili kuanzia Agosti 11-12, 2022.
Awali akisoma taarifa ya makusanyo ya kodi kwa mikoa hiyo ya kanda ya ziwa, Bw.Hashim Ngoda ambaye ni Meneja wa TRA Mkoa wa Geita amesema, kwa mwaka wa fedha 2022/23 hususan mwezi Julai, Mikoa ya Kanda ya Ziwa ilipangiwa kukusanya Bilioni 30.7 na kufanikiwa kukusanya zaidi ya Bilioni 35 sawa na asilimia 115, huku Geita pekee ikiongoza kwa kukusanya kwa asilimia 183.
Bw.Ngoda vilevile, amweleza RC Shigela juu ya changamoto zinazoikabili Geita zikiwemo Wafanyabiashara kutokutoa risiti za EFD, wananchi kutozidai risiti hizo, upitishwaji bidhaa kimagendo hali ambayo hupelekea kupoteza mapato ya ushuru wa forodha hali ambayo husababisha ushindani usio na uwiano sahihi lakini pia kuomba kusaidiwa na maafisa masuhuli kukusanya kodi ya zuio wanapofanya kazi na Wafanyabiashara, mambo ambayo RC Shigela ameahidi kuwekea msisitizo kama ambavyo ameombwa na TRA.
Naye Katibu Tawala Mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara ametumia nafasi hiyo kujitambulisha kwa watendaji hao ikiwa ni mwendelezo wa kujitambulisha kwa watendakazi mkoani Geita na kisha kuipongeza TRA Geita kwa kuongoza kwenye kanda kwa mwezi Julai kwa kukusanya asilimia 183 ya lengo.
Jiandae Kuhesabiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa