Hatimaye mkutano wa uboreshaji utoaji huduma za afya zenye kuzingatia heshima, staha na haki za jinsia kwa afya uzazi, mama wajawazito, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano na huduma uliozishirikisha Halmashauri za Wilya na Mji Geita waja na makakati wa kuboresha afya ya mama na mtoto, si mwingine bali ni mkataba wa huduma kati ya mteja na watoa huduma za afya, mkutano uliofanyika wa siku mbili kuanzia tarehe 29-30.08.2018 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Akifunga mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita Bi Janeth Mobe ameishukuru USAID Boresha Afya kwa kushirikiana na serikali kuleta mkutano huo wenye mafunzo kadha wa kadha na kukiri uwepo wa uelewa wa pamoja baina ya viongozi walioshiriki wakiwemo wa kidini na kisiasa na kuwaasa washiriki wa mkutano kuyafanyia kazi waliyoelekezwa.
Amesema,“tulichokipata hapa tusikiache hapa, lakini pia binafsi ingawa si mtaalamu wa afya ila nimejifunza mengi”. Amewaeleza watumishi wa afya kwenda kufanya kazi kwakuwa wao ni mabalozi ndio maana wamechaguliwa kwa niaba ya wenzao. Lakini pia amewaasa kutokaa kimya endapo watanyanyasika katika maeneo yao ya kazi kwani ofisi ya Mkuu wa Wilaya ipo tayari kuwasadia. Bi. Janeth pia akatumia fursa hiyo kuwasihi wahudumu wa afya kuwa na moyo mnyenyekevu na wa kipekee wanapowapokea wagonjwa kwani bila Mungu kazi yao ni ngumu. Akamaliza kwa kuwaomba watumishi wa afya kuwa na umoja na ushirikiano wanapofanya kazi ya kuhudumia wananchi na kuepuka ucheleweshaji wa huduma kwa akinamama wajawazito na watoto ili kuokoa maisha yao.
Kwa upande mwingine, washiriki wa kikao wamewaomba viongozi wa siasa wawapende watumishi na siyo kuwalaumu kama ambavyo imekuwa ikijitokeza kwa baadhi ya maeneo na kupongeza viongozi ambao wamekuwa wakiwatembelea watumishi na kuwatia moyo ili waendelee kufanya kazi kwa bidii.
Washiriki pia walipata fursa ya kuupitia mkataba (kwa makundi) unaopendekezwa kutumika kati ya mteja na watoa huduma za afya na kisha Afisa wa Masuala ya Jinsia na Vijana Mradi wa USAID Boresha Afya ndugu. Revocatus Kadoshi akawaeleza taratibu zitakazofuatwa ili kuanza rasmi matumizi ya mkataba huo akisema; “Mkataba unaotarajiwa kutumika kama nyenzo ya kuboresha huduma za afya kwa mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano utaleta manufaa si tu kwa walengwa wa mradi bali hata na jamii isiyolengwa na mradi kwakuwa pale mtoaji na mpokea huduma wanapojua haki na wajibu wao, ni dhahiri kuwa uwajibikaji utakuwepo kwa pande zote.
Baada ya mkataba huu kupitiwa na RHMT na CHMT, utapelekwa kwa mwanasheria kwa ajili ya kuupitia na kushauri kitaalamu, kisha kuurudisha kwa wajumbe hao. Baada ya hatua hiyo, Mganga Mkuu wilaya na Katibu wa Afya watawasilisha mkataba huo kwa Kamati ya Elimu, Afya na Maji, kisha kama una marekebisho kurudi kwa wataalamu tena na endapo utapitishwa, utapelekwa kwenye Baraza la Madiwani. Ikiwa Baraza litaridhia, basi Mkurugenzi Mtendaji/Mkurugenzi wa Mji atausaini mkataba huo, tayari kutekelezwa kwenye halmashauri husika. Mradi utagharamia machapisho ya mkataba huo na kuusambaza lakini pia kuuweka Mkataba kwa kifupi kwenye mabango (poster) kwenye vituo vya kutolea huduma za afya yani zahanati, kituo cha afya na hospitali.
Jukumu la kuielimisha jamii ni la viongozi wa dini na siasa ambao hawa hukutana na jamii mara kwa mara na endapo watahitaji msaada wa kitaalamu basi watasaidiwa na wataalamu waliopata maelekezo kupitia mkutano huo.
Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Geita ndugu Peter Tango akawashauri timu iliyoshiriki mkutano huo, kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wenzao walioko vituoni lakini kuwa na mawasiliano ya karibu ili kusaidiana pale panapokuwa na changamoto.
Mkutano umeaihirishwa na utaendelea katika halmashauri zilizobaki ndani ya Mkoa wa Geita.
“tuungane pamoja kuzuia vifo vya mama na mtoto”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa