Leo tarehe 29.08.2018 umefanyika Mkutano wa Wadau wa Utetezi na Ushawishi wa Utoaji Huduma za Afya zenye kuzingatia heshima, staha na haki za jinsia kwa afya ya uzazi, mama wajawazito, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano na huduma rafiki kwa vijana utakaodumu kwa siku mbili katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Akifungua mkutano huo Bi. Janeth Mobe kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Gieta amesema kuwa, ni vyema kina baba kushirikishwa katika kuilinda afya ya mama na mtoto ndipo mradi huu utafanikiwa.
Amesema, “upo umuhimu mkubwa wa kumshirikisha baba ili awe na uelewa juu ya umuhimu wa afya ya mama na mtoto, jambo hili litawezesha kampeni hii ya kuboresha afya iweze kufanikiwa na kuondoa dhana potofu isiyozingatia haki za jinsia kwa afya ya uzazi, mama wajawazito n.k”.
Naye ndugu Revocatus Kadoshi ambaye ni Afisa wa Masuala ya Jinsia na Vijana wa Mradi wa USAID Boresha Afya amesema, lengo la mkutano huo ni kuja na mkakati unaombatana na mkataba wa huduma kwa mteja utakaokuwa na vipengele vya Haki na Wajibu. Kwamba, Katika mkataba huo, mtoa huduma atatakiwa kutambua haki na wajibu wake akiwa kazini akitoa huduma, lakini vilevile mteja ama mpokea huduma pia atatakiwa kujua wajibu na haki yake ili kuondoa malalamiko kadha wa kadha yanayotokea kutokana na pande hizi kutokuwa na uelewa wa pamoja wa haki na wajibu.
Katika wasilisho lake, ndugu Kadoshi ameeleza uwepo wa mradi huo ndani ya mkoa mzima wa Geita, yaani kwenye Halmashauri zote sita za mkoa na kwamba mradi huo umeanza kutekelezwa kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2016 na utaisha mwezi Septemba mwaka 2021 ambao unatekelezwa katika mikoa 6 ya kanda ya ziwa na mkoa mmoja wa kanda ya magharibi ambao ni Kigoma.
Miongoni mwa jambo lililogusiwa ni pamoja na wataalamu wa afya kukerwa na tabia ya wakunga wa jadi kuwarubuni akinamama wajawazito kwa kuwapa madawa ya kienyeji yenye madhara wakati wa kujifungua jambo ambalo linawapa wakati mgumu pindi wanapowahudumia akinamama hao muda huo wa kujifungua hivyo kuomba wakunga hao kuacha kazi hiyo ya kitaalamu ifanywe na wataalamu.
Mwisho, mkutano huo unategemewa kuja na matokeo yatakayoviwezesha vituo vya kutolea huduma za afya na jamii kwa pamoja kusaidiana kuboresha na kulinda uhai wa mama wajawazito na watoto ikiwa ni pamoja na namna ya ushirikishwaji wanaume ili kuepusha madhara mengi yatokanayo na mfumo dume pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya afya kwenye jamii.
Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ni Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, Uongozi wa Hospitali ya Mkoa, Wataalamu wa Afya ngazi za Halmashauri, Wawakilishi wa Wabunge, Viongozi wa Dini, Maafisa Habari na Maofisa wa Mradi wa USAID Boresha Afya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa