Ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazokwamisha Kampeni ya Usafi wa Mazingira Mkoani Geita, kimeendeshwa kikao cha kubadilishana uzoefu wa utekelezaji wa kampeni hiyo baina ya wataalam wa Kamati za Elimu, Afya na Maji na wadau (WEDECO) kutoka Halmashauri 6 za Mkoa wa Geita, kikao kilichofanyika tarehe 09.01.2019 katika Ukumbi wa Mikutano, Hospitali ya Wilaya Bukombe chini ya uratibu wa Bw.Elisante Shumbi, Afisa Afya wa Mkoa wa Geita.
Akisoma hotuba ya ufunguzi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Immaculata Raphael amewashukuru wajumbe kwa kuhudhuria, huku akiwataka kuwa na ushirikiano wakati wa kutekeleza kampeni hiyo, ambapo katika taarifa ya mkoa imeonesha kuwa bado utekelezaji si wa kuridhisha kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo uhamasishaji wa matumizi ya choo bora, uundwaji wa kamati za usafi na mazingira shuleni, upatikanaji wa miundombinu ya Usafi katika shule hasa za msingi n.k
Amesema ,“ ni wakati sasa wa kuhakikisha mnafanya kazi kwa kushirikiana, vyoo vijngwe palipo na mtandao wa maji ili dhana ya vyoo bora ionekane, na ni kwa kushirikiana ndipo mtaalam wa elimu, maji na afya wataweza kufanikisha suala hili. Lakini pia ni muhimu kuunda klabu za kutosha mashulrni ili kampeni hii itekelezwe mashuleni kwa usahihi”
Pia, Mhandisi Raphael anatoa wito kwa kamati kufanya ukaguzi wa kiafya katika kambi mbalimbali za machimbo ya madini zinazoibuka kila wakati kwa lengo la kuthibiti uchafuzi wa mazingira kwa kuhakikisha kunakuwepo vyoo na miundombinu ya usafi, lakini pia usalama mahala pa kazi unazingatiwa na kuwahimiza watumishi kuendelea kuheshimu maelekezo yanayotolewa wakati fedha zinapoletwa ili kufanya kazi kusudiwa.
Wajumbe walipatiwa pia elimu juu ya usalama wa chakula na uthibiti wa magonjwa ya kuambukiza kutoka kwa Afisa ayfa na Mratibu wa Magonjwa ya Kuambukiza Mkoa wa Geita Bw. Jimmy Mtabwa, elimu iliyokumbusha juu ya kutotumia vyakula vilivyomaliza muda wake (expired), kupenda kupika chakula kitakachoisha siku moja yani kutopenda kula viporo na bila kuvipasha n.k
Mwakilishi wa WEDECO Bw. Gwamaka Mwasandende, kwa upande wake alipendekeza kuwa, ni vyema wadau kuwa wanaendelea na mradi pale aliyetangulia atakapokuwa ameishia kuliko kila mdau anakuja na kuanza upya, jambo linalopelekea kurudi nyuma katika utekelezaji
Mwisho, wajumbe waliweza kujadiliana masuala kadha wa kadha na kuahidi kukamilisha yale yote waliyojipangia ikiwemo utengaji wa maeneo ya kuhifadhia taka, lakini pia kushindanisha vijiji katika upatikanaji wa kaya zenye choo bora kwa lengo la kuhamasisha usafi wa mazingira, ikiwa kubwa zaidi kuwa na ushirikiano wakati wa utekelezaji, kufanya kazi kama timu moja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa