Katibu Tawala Mkoa wa Geita Ndg.Mohamed Gombati amebainisha kuwa ushirikiano wa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyagh'wale, wazazi na walimu umefanya Kuongezeka kwa ufaulu mwaka 2025 Ukilinganisha na Ufaulu wa Mwaka 2024 wa matokeo ya Darasa la Saba wilayani humo.
Ndg. Mohamed Gombati ameyasema hayo wakati wa hafla ya utoaji motisha kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma, hafla iliyofanyika Katika Shule ya Sekondari Msalala iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Nyagh'wale tarehe 4 Disemba 2025.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ameeleza kuwa wanafunzi waliofanya vizuri wamedhihirisha mojawapo ya faida ya elimu ambayo ni kutengeneza kujiamini na kujenga uwezo wa kuisaidia Serikali katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya maendeleo.
Ndg.Gombati ametoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyagh’wale kuendelea kuwapa lishe wanafunzi Ili ufaulu uweze kuongezeka. Pia amewasisitiza wazazi na walezi kuwalea watoto katika maadili mema yanayokubalika katika jamii.
Katibu Tawala Wilaya ya Nyagh'wale Bi.Kaunga Amani amesema waliunda tume ya Kufuatilia changamoto za elimu na baada ya kuzibaini wakazifanyia kazi kwa kushirikiana na walimu na kuyafanyia kazi maelekezo ya kamati ya usalama wilaya, miongoni mwa maelekezo hayo ni kulima zaidi ya hekari mbili zitakazowezesha upatikanaji wa chakula mashuleni na kuondoa tatizo la utoro kwa wanafunzi.
Mwakilishi wa Afisa Elimu Mkoa wa Geita Ndg.Salome Cherehani amewapongeza walimu na wanafunzi waliofanya Vizuri katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi na amewasisitiza kuendelea kufanya vizuri katika elimu ya Sekondari bila kusahau kuwa watiifu na wenye nidhamu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Nyagh'wale Bi.Husna Toni amesema madhumuni ya Hafla hiyo ni kuwapongeza walimu waliofaulisha wanafunzi vizuri kwa alama A kwa masomo yote kwa Kuwapatia motisha ya Zawadi mbalimbali kwa lengo la kuwatia moyo walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyagh'wale Bw. Nassoro Hamisi amesema ufaulu wa mwaka 2025 umeongezeka tofauti na Mwaka jana hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Nyagh'wale imeamua kutoa motisha kwa walimu Ili kuwaongezea nguvu waweze kufundisha kwa weledi na kupelekea kupatikana kwa matokeo mazuri kila mwaka.
Mbunge wa Jimbo la Nyagh'wale Mhe.Hussein Kasu amesema yupo tayari kutoa kilo 200 za mbegu za mahindi na maharage kwa shule zote za sekondari na msingi wilayani humo na kuwasisitiza wazazi na walezi kuwasimamia watoto Ili waweze kuwa na Maendeleo mazuri katika masomo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake waliofanya Vizuri mhitimu wa darasa la saba mwaka 2025 Abigael Richard Mwisaji amewashukuru walimu, wazazi na walezi kwa Msaada wao mkubwa katika kuhakikisha wamepata matokeo mazuri aidha amewasisitiza wanafunzi wenzake wanaoendelea na masomo mashuleni kuweka msisitizo katika elimu ili iwakomboe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa