Uzinduzi rasmi wa Dawati la Huduma za Ustawi wa Jamii katika Kituo kikuu cha mabasi Geita Mjini kutawezesha watoto na watu wote wanaopitia vitendo vya kikatili katika maeneo ya stendi kupata msaada wa kitaalam pindi wanapokutana na changamoto hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Stephen Mwaisobwa alipokuwa akizindua rasmi Dawati la Huduma za Ustawi wa jamii ambalo limeanzishwa na Shirika la Railway Children Africa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Geita pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita katika eneo la Stendi kuu ya mabasi Geita mjini tarehe 07/8/2025.
Dkt. Stephen Mwaisobwa ameeleza kuwa ili kulinda ustawi wa watoto, ushirikiano wa hali ya juu unahitajika baina ya jamii na viongozi wengine wa Serikali kuanzia ngazi ya mtaa au kijiji. Pia amewasihi wananchi kutimiza wajibu wao kwa kila mlezi/mzazi na kuhakikisha Dawati lililoanzishwa katika eneo la stendi kinatumika ipasavyo kwa watumiaji wa stendi kutoa taarifa za mianya au vitendo vya kikatili vinavyofanyika katika eneo hilo.
Meneja wa Shirika la Railway Children Kanda ya Ziwa Ndg. Irene Wampembe amesema kuwa lengo lao katika kuanzisha Dawati hilo ni kuhakikisha eneo la umma linakuwa salama kwa watoto na watu wote wanaokumbana na changamoto wakati wa harakati za usafiri.
Ndg. Wampembe ameongeza kuwa walengwa waliokusudiwa kuhudumiwa na Dawati hilo ni watoto na watu wazima wanaopitia vitendo vya ukatili hususan wanaotelekezwa katika vituo vya mabasi, watoto wanaoishi mitaani, watoto na watu wazima wanaosafiri peke yao bila uangalizi wowote,wafanyakazi wa ndani wanaofika stendi kuomba msaada wa kurejeshwa nyumbani kwao, watu wazima wenye matatizo mbalimbali ambao wakienda mikoani kufuatilia stahiki zao wanalala stendi kutokana na sababu ya kukosa eneo la kufikia pamoja na watoto, vijana na mtu yeyote aliyekimbia vitendo vya ukatili.
“Sambamba na majukumu mengine, Shirika letu kwa kushirikiana na wataalam wengine tutaendelea kutoa elimu kwa jamii ili waelewe umuhimu wa kuwa na Dawati la Ustawi wa jamii katika eneo la Stendi ya mabasi Geita. Pia linawawezesha Maafisa Ustawi wa jamii ili waweze kuwasafirisha watoto wa mitaani waliobainishwa kurudi majumbani kwao na kudhibiti ongezeko la wimbi wa watoto wa mitaani pamoja na kupambana na vitendo vya kikatili na unyanyasaji vinavyofanyika kwenye jamii.” Aliongeza Ndg. Irene Wampembe.
Akitoa taarifa ya idadi ya watoto wa mitaani waliobainika katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Mei 2025, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Geita Bw. Frank Moshi amesema kuwa jumla ya watoto 169 walibainishwa katika wilaya zote za Mkoa wa Geita huku asilimia kubwa ikionesha ni watoto waliotoka katika maeneo ya mjini ambapo ni makao makuu ya wilaya. Watoto hao walirudishwa mikononi mwa familia zao, baadhi kukabidhiwa katika vituo vya kulelea watoto na wachache kurejeshwa Mikoa ya jirani walipotokea kabla ya kukimbilia Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa