Makundi maalum ambayo yanajumuisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wamekumbushwa kuunda vikundi vitakavyowawezesha kupatiwa mitaji kutoka kwenye fedha za asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri zinazotolewa ili kuwakwamua watu hao kiuchumi.
Wasia huo umetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ndg. Ismail Ali Ussi alipokuwa akizungumza na vijana pamoja na wananchi wengine waliojitokeza katika Mbio za Mwenge wa Uhuru ulipotembelea kikundi cha vijana wataalam wa ufanisi katika Kijiji cha Ibambila Kata ya Nyang’hwale tarehe 03 Septemba 2025.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita imeondosha changamoto ya vijana kulalamika kukosa mitaji kwa kutoa fursa ya mikopo ya asilimia 10% hivyo ni jukumu la vijana kujiunda katika umoja utakaowawezesha kupata mitaji ya kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kutoka Halmashauri.
“ Vijana achene kulalamika kutokana na ukosefu wa ajira na ukosefu wa mitaji na badala yake mnatakiwa kubuni mbinu mpya za utafutaji wakati Serikali ikiwashika mkono kwa kutoa mikopo nafuu kwa ajili ya kuendeleza na kukuza mitaji yao.” Aliongeza Ndg. Ismail Ali Ussi.
Akieleza faida za mradi huo Katibu wa Kikundi cha vijana wataalam wa ufanisi amesema kuwa mradi huo umeweza kukuza uchumi kwa wanakikundi na kuongeza kipato cha familia zao, kutoa ajira kwa watu wengine wakiwemo mama lishe, wauza mbao na vijana wa ulinzi, kutoa mafunzo kwa vijana wengine juu ya ufundi pamoja na kufanya kazi na taasisi za Serikali ikiwemo Halmashauri kupitia kazi zinazotangazwa kwenye mfumo wa NEST.
Mwenge wa Uhuru 2025 umebeba kauli mbiu isemayo” Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu”. Aidha pamoja na ujumbe huo Mbio za Mwenge wa Uhuru unahamasisha wananchi kupambana na rushwa, kuzuia ugonjwa wa Malaria, mapambano dhidi ya UKIMWI na matumizi ya Dawa za kulevya na kuwaelimisha wananchi juu ya kuzingatia lishe bora.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa