Tarehe 19.02.2019, wakazi na wananchi wa Mkoa wa Geita wameendelea kuhakikishiwa usambaziwaji na uwashiwaji wa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini REA, wakati wa ziara ya siku mbili mkoani hapa ya Waziri wa Nishati Mhe.Dkt.Medard Kalemani (Mb).
Hayo yamedhihirika baada ya Mhe. Dkt. Kalemani kuwasili Mkoani Geita akieleza lengo mahsusi la ziara yake, alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ofisini kwake na kutoa pongezi za utendaji kazi kwa Mkoa wa Geita kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika na kumuomba kutosita kuwasilisha changamoto za nishati umeme kwa kadri zitakavyojitokeza.
Amesema, “kwanza nifikishe salamu za Mhe. Rais Magufuli kwa wanageita, anawasalimu sana na anawapongeza Geita mnafanya kazi. Nimekuja na wenzangu kufuatilia utekelezaji wa miradi ya REA, ambapo kwa sasa tupo katika hatua ya katikati ya utekelezaji huo ikiwa ni miezi 5 tangu Septemba 2018 kwa mkataba wa miezi 24, lakini pia kufuatilia hali ya kiumeme ndani ya Mkoa wa Geita na tunatambua bado haujaimarika kiasi cha kutosha, changamoto tunaendelea kuzipunguza lengo zitatuliwe na wananchi wanufaike na huduma ya umeme”.
Ameendelea kusema kuwa, kwa siku mbili (2) akiwa Geita, vijiji kumi na mbili (12) vitawashiwa umeme ambapo kwa Wilaya Geita kutakua na vijiji vine (4) likiwemo Gereza la Butundwe, ambalo kwa muda mrefu limekuwa gizani, hivyo watanzania walio gerezani watafurahia umeme kuanzia leo.
Mhe.Dkt. Kalemani amemhakikishia Mkuu wa Mkoa juu ya ufikishaji wa umeme kwenye nyumba za watumishi na majengo ya ofisi za serikali zilizopo eneo la Magogo, lakini pia umeme utaendelea kufikishwa kwenye maeneo yote yenye uzalishaji wa dhahabu ili wananchi waweze kuchangia pato la taifa huku shirika nalo likipata faida.
kwa wale wote waliorukwa na umeme wa REA kwa namna moja ama nyingine, wameahidiwa kuangaliwa kwa utaratibu mwingine ili nao waweze kupata huduma hiyo muhimu, hivyo ameendelea kuomba ushirikiano kutoka kwa wananchi
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel alimkaribisha Mhe. Dkt. Kalemani akimuomba kufikisha salamu kwa Mhe. Rais Magufuli na kupongeza utendaji wa Wizara ya Nishati wa kasi katika kuhakikisha Tanzania ya Viwanda haikwami, lakini pia wananchi wanapata umeme, kisha kuomba umeme ufikishwe kwenye eneo la Magogo zilipojengwa nyumba za watumishi, hospitali pamoja majengo ya ofisi za serikali ikiwemo jengo la utawala Halmashauri ya Mji Geita.
Mradi wa REA awamu ya Kwanza unatarajiwa kukamilia ifikapo Juni, 2019 na kwa Mkoa wa Geita wenye vijiji 210, vijiji 45 kwa miezi mitano ndivyo tayari umeme umekisha washwa na 12 vitakavyowashwa leo vitafikisha jumla ya vijiji 57, na kwamba bado lengo ni kumaliza changamoto zote za nishati umeme. Kwa Nchi nzima vijiji 62 vinatarajiwa kuwashiwa umeme leo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa