Shirika lisilo la Kiserikali la VSO Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Mkoa wa Geita SIDO wamewazesha jumla ya vijana wajasiriamali 35 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 vifaa mbalimbali ili waweze kujikwamua kiuchumi baada ya kuwapa mafunzo ya wajasiriamali.
Hafla hiyo imefanyika Februari 24, 2022 katika ukumbi wa zamani wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka VSO, SIDO, Geita RS, Benki ya NMB Halmashauri za Geita na vikundi vya sanaa na burudani.
Akiongea kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw.Musa Chogero ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita amewapongeza wote walioshirikiana kwa kuiunga mkono serikali kulisaidia kundi hilo la vijana kwani kwa kufanya hivyo ni kuongeza wigo wa kujitegemea katika uzalishaji na hivyo kuisaidia nchi kukua kiuchumi huku akiwataka vijana hao kuepuka tamaa ya fedha ili kuzingatia maadili na ubora wa bidhaa.
“niwapongeze VSO, SIDO, Halmashauri za Geita na wadau wote zikiwemo taasisi za kifedha kwa kuwasaidia vijana hawa kwani kwa kufanya hivi kuunga mkono juhudi za serikali kama ambavyo nayo hutoa 10% ya mapato ya ndani ya halmashauri kuwezesha makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu, kwetu ni faraja kuona wajasiriamali hawa wanaongezeka. Siwezi kuacha kuwapongeza pia vijana kwa bidhaa nzuri zinazovutia, hongereni sana maana nimepita nimeziona bidhaa zenu”. Alisema Bw.Chogero
Katibu Tawala Huyo aliongeza kuwa, “ni vyema VSO mtufikshie shukran za dhati kwa wafadhili kutoka nchi ya Uholanzi na kwa hakika niwakumbushe wote tukumbuke kutunza mazingira yetu katika shughuli zetu kama ambavyo tumeelezwa juu ya kundi lililowezeshwa kutengeneza mkaa mbadala”. Alimaliza kwa kuwasihi taasisi za kifedha kubuni masharti nafuu ili kuwawezesha wajasiriamali hao kukopa kwenye benki hizo za NMB na NBC kisha kuzindua shughuli hiyo kwa kukata utepe na kugawa vifaa hivyo vilivyotolewa bure kwa wajasiriamali hao.
Wakitoa maelezo ya mradi, Meneja Mradi wa Clarity Bw. Elvis Chuwa na Mwakilishi wa Meneja wa SIDO Geita Bw.Bakari Kitobori wamesema, mafunzo hayo yalitolewa kwa vijana 35 ambapo 8 walipewa mafunzo ya ushonaji nguo, 8 walipewa mafunzo ya utengenezaji wa sabuni na batiki, 8 walipewa mafunzo ya usindikaji wa vyakula mbalimbali na 8 walipewa mafunzo ya ufugaji wa kuku, utengenezaji chakula cha mifugo na 3 walipewa mafunzo ya utengenezaji mkaa mbadala.
Viongozi hao wawili walieleza kuwa, mafunzo hayo yalichaguliwa na vijana wenyewe na hivyo wanaamini kupitia wao,vitazalishwa viwanda vidogo vingine vingi na wanaamini vijana hao wataongeza masoko kutokana na elimu waliyoipata.
Kabla ya kuanza kwa shughuli hiyo, mgeni rasmi alipita na kupewa maelezo juu ya bidhaa zilizotengenezwa na vijana hao baada ya kuwezeshwa mafunzo ya ujasiriamali kutoka SIDO kwa uwezeshwaji wa VSO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa