WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI WATAKIWA KUSITISHA AJIRA ZA WATOTO
Wachimbaji wadogo wa madini Mkoani Geita wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kuajiri watoto wadogo kushiriki katika migodi midogo midogo iliyopo mkoani hapa kwa kuwa watoto hao wanatakiwa kuwa shule.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya wachimbaji wadogo wa madini iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe Ezekiel Kyunga Mkuu wa Mkoa amewataka wachimbaji hao kuhakikisha hawatoi ajira kwa watoto wadogo katika maeneo yao ya migodi kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha na kuwanyima fursa ya kupata elimu. “kumekuwa na tabia ya kuajiri watoto wadogo katika maeneo mengi ya migodi tambueni kuwa watoto hao wanakosa masomo na pia mnahatarisha afya zao, hatua kali zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakaye ajiri watoto katika mgodi wake’’.
Aidha, amewataka wachimbaji hao kuhakikisha wanakuwa na mpango mzuri wa kutunza mazingira katika maeneo ya shughuli za uchimbaji wa madini ili kuhifadhi mazingira ili baadae wakati wa ukomo wa mgodi mazingira yabaki katika hali nzuri. Amewasisitiza wachimbaji wadogo kutumia elimu waliyoipata kuwaelimisha wachimbaji wengine ili kuboresha shughuli za uchimbaji wa madini ili kuweka hali nzuri ya usalama katika migodi kwa kuwa siku za hivi karibuni migodi imekuwa ikiporomoka mara kwa mara. Ameongeza kuwa kazi ya serikali ni kusimamia na kutoa elimu ili uchimbaji uwe katika hali nzuri hivyo wazingatia mafunzo hayo wakati wa utekeezaji wa shughuli zao za uchimbaji wa dhahabu. Vile vile amesema kuwa wakati umefika kwa Mkoa wa Geita kuwa na maduka ya vifaa vya uchimbaji wa madini pamoja na maduka ya Dhahabu kwa kuwa hakuna Mkoa hapa nchini wenye madini mengi ya Dhahabu kama ilivyo Geita hivyo, amewataka STAMICO na Kamishina wa madini kufuatilia ili huduma hizi muhimu zipatikane mkoani Geita.
Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya madini Mkoa wa Geita na kufadhiliwa na shirika la Plan International wachimbaji wadogo wameishukuru serikali na wadau hao kutoa mafunzo hayo ambayo kwao yana manufaa makubwa na watayatumia kuboresha shughuli za uchimbaji ulio salama na unaozingatia sharia na utunzaji wa mazingira.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa