Viongozi na wawakilishi wa wananchi kwa ngazi za Halmashauri, kata na vijiji wakiwemo waheshimiwa madiwani wameshauriwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao na mashirika mbalimbali inafanyika kama ilivyokusudiwa walipokuwa kwenye kikao cha wadau juu ya maendeleo ya mradi wa majisafi na usafi wa mazingira uliyopo kwenye Halmashauri za Wilaya ya Geita na Nyang’hwale.
Hayo yameelezwa na Eng. Immaculata Raphael aliyefungua kikao hicho, wakati akisoma hotuba kwaniaba ya mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Geita akiwakumbusha washiriki wa kikao hicho kuwa wanapaswa kutambua mradi huo unaelekea ukingoni, hivyo ni vyema kutumia vizuri muda na nafasi iliyopatikana katika utekelezaji wa mradi huo, huku akiwapongeza madiwani waliohudhuria kikao hicho kwa wingi na kuwashukuru watekelezaji wa mradi huo unaoshirikiana na serikali.
Amesema “nawashukuru sana waheshimiwa madiwani kwa kuhudhuria kwa wingi katika kikao hiki muhimu, vile vile niwashukuru wadau mnaoshiriki kutekeleza mradi huu. Niwaombe viongozi tutambue yakuwa muda si rafiki na unakaribia kuisha kwakuwa mradi ni wa miaka minne tangu mwaka 2016, hivyo tujipange kuendeleza pale wadau watakapoachia kwakuwa ni dhahiri kuwa hata wengine nao wanahitaji msaada wao”.
Eng. Raphael amewakumbusha wajumbe hao juu ya umuhimu wa kutambua kwamba lengo la mradi ni kupunguza vifo vya kina mama na watoto vitokanavyo na uzazi kwa kuboresha miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya na kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama bila kusahau kuinua kiwango cha usafi wa mazingira ngazi ya kituo cha afya, shule na kaya zinazozunguka kituo, kisha kuweka kikao wazi akiamini kikao hicho kitatoa mapendekezo ya namna bora zaidi ya kuboresha utekelezaji wa mradi huu na hatimaye kupunguza vifo visivyo vya lazima.
Akiongea kabla ya hotuba ya ufunguzi, Dkt. Greyson Mbaruku ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Shirika la WEDECO amewaeleza wajumbe hao kuwa, ni vyema wakawa huru kuchangia mawazo yao katika kuboresha utendaji wa mradi huo.
Nao waheshimiwa madiwani kama viongozi wa kisiasa na wenye nafasi kubwa ya ushawishi kwenye jamii wakiongozwa na wenyeviti wa Halmashauri hizo, wameshukuru kwa uwepo wa mradi huo na kupongeza juhudi zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau, wakiahidi kuhakikisha kwenye halmshauri wanazozisimamia wanatenga fedha ili kuendeleza juhudi hizo zilizoanzishwa, kisha kuomba wadau hao wendelee kutoa ushirikiano na hata pengine kuleta miradi mingine Geita.
Mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira unafadhiliwa na nchi ya Canada na kutekelezwa na mashirika ya Amref Health Africa na WaterAid Tanzania, ambapo Amref wanahusika na mafunzo ya wauguzi, ujenzi wa majengo na utoaji vifaa tiba na lishe wakati WaterAid hushirikiana na wadau wa maendeleo WEDECO Ltd katika upatikanaji wa maji safi na salama, bila kusahau mafunzo ya usafi wa mazingira na tendanishi (usafi binafsi).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa