Walimu na viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kanda ya ziwa wamekumbushwa juu ya wajibu walionao wa kuielimisha jamii juu ya wapi nchi ya Tanzania imetoka, ilipo na inapokwenda ili kuwa na taifa la wazalendo wanaoipenda nchi yao na kwamba, watambue kihistoria mwalimu ni mkombozi wa taifa hili kupitia Hayati Mwl.Julius Nyerere.
Hayo yalielezwa ijumaa ya Agosti 16, 2020 na mkuu wa mkoa wa geita mhandisi Robert Gabriel alipokuwa akifungua warsha ya makatibu na makatibu muhtasi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wa mikoa ya kanda ya ziwa ya Mara, Mwanza, Geita na Kagera iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa JJ Hotel uliyopo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro wilayani Geita.
Alisema, "msijidharau, ninyi ni wa pekee kwani hata ukombozi wa taifa hili uliletwa na mwalimu, hivyo ni imani yangu kwenu kuwa mnao wajibu wa kuieleza jamii tulipotoka, tulipo na tunapoelekea kwani kwa kufanya hivyo tutalisaidia sana taifa hili kuwa la wazalendo na wenye mshikamano kama ilivyo kaulimbiu yenu" kisha kuwaombea mafanikio akijipambanua zaidi kama shemasi wa mkoa.
Aliongeza kuwa, mwalimu ni kioo cha jamii, kioo cha taifa, mtu ambaye kazi yake hudumu milele na kwamba walimu wanapaswa kuyaenzi yale mema na misingi aliyoiacha baba wa taifa kwani misingi inapokuwa imara, maisha ya mtanzania huboreka na ndiyo maana hata kwa juhudi za kiongozi wa nchi yetu wa sasa ambaye pia ni mwalimu, amepambana na kutuvusha kwenye janga la korona kwa kumuomba Mungu lakini pia kutuvusha na kuingia uchumi wa kati .
kipekee mhandisi Gabriel aliwaeleza viongozi na watendaji hao kuwa, ndani ya kipindi kifupi Geita itakuwa ni mji wa kipekee, ikiwa kwa mwezi wa septemba, 2020 soko kuu la dhahabu lililopo mjini Geita liliendesha biashara ya Bilioni mbili kwa mwezi, huku ujenzi wa soko jingine la kisasa ukiendelea katika mamlaka ya mji mdogo katoro na kuwaeleza kuwa kila wilaya imepangwa kuwa na soko zuri la kisasa la biashara hivyo kuendelea kuwakaribisha wananchi wote kuwekeza mkoani hapa.
Akitoa neno la shukrani, katibu wa CWT mkoa wa Mwanza mwl. Daniel Mafwili alimshukuru na kumwomba mkuu wa mkoa kufikisha salamu zao kwa mhe.Rais Magufuli kwani amekuwa msikivu sana kwao na kwamba wanamuombea afya njema, lakini vile vile kuwapuuza wanaozusha na kudanganya umma kwa maneno mbalimbali juu ya kutokupanda kwa mishahara ya walimu na kwamba wao wanaamini wataendelea na majadiliano kwa kila changamoto itakayojitokeza na si kuhamasisha maandamano kisha kumaliza kwa kusema, "kupanga ni kuchagua"
Warsha hiyo hufanyika mara moja kila mwaka ilihudhuriwa pia na wadau wa NSSF na NHIF Geita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa