Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela ametoa hamasa kwa wananchi wa Geita kutumia raslimali zinazopatikana Nchini na fursa zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi wao binafsi na jamii inayowazunguka.
Mhe. Shigela ametoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa akizindua rasmi Kongamano la kuhamasisha uwekezaji wa ndani katika Mkoa wa Geita lililofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Kongamano hilo limeandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo maalum ya kiuchumi Tanzania (TISEZA).
Mkuu wa Mkoa wa Geita ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwezesha sekta mbalimbali za uzalishaji kama kilimo ambapo kwa Mkoa wa Geita mradi wa umwagiliaji Ibanda ambao utahitaji maghala ya kuhifadhia mazao, mashine za kisasa za kuvunia mpunga na kukoboa na miundombinu mingine muhimu ambayo yote ni fursa zinazoweza kutumiwa na wananchi.
Mhe. Shigela ameongeza kuwa kampeni inayofanywa na TISEZA itawasaidia wachimbaji wengi wa Madini kufanya uwekezaji kwa ubia stahiki pasipo kukiuka sheria, kanuni na taratibu za Nchi na kufafanua kuwa wachimbaji wadogo wengi wanawekeza kwa mazoea kwa kutofahamu taratibu zinazohitajika, jambo ambalo huenda likabadili mitazamo na kuongeza uzalishaji kwa maslahi mapana ya Mkoa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TISEZA, Balozi Dkt. Azizi Mlima amesema kupitia kampeni ya uwekezaji wa ndani Mamlaka yake imelenga kubadili fikra kwa wananchi walio wengi ni kufikiri kuwa uwekezaji mahsusi ni wanaotoka nje ya Nchi lakini watanzania wanatakiwa kutumia fursa zilizopo Nchini kufanya uwekezaji mdogo, kati na mkubwa.
Kwa upande wake Meneja na Msimamizi wa Mradi wa nishati safi ya kupikia Bw. Hamisi Yahaya amesema kuwa jambo ambalo amejifunza kutoka kwenye kampeni hiyo na kuwashauri wachimbaji Madini kujisajili kama wanachama wa TISEZA na kunufaika na msamaha wa kodi ya forodha kwa aslimia 100% watakapohitaji kuagiza vifaa vya kazi kama mashine za CIP, malori makubwa ya kubeba marudio, mashine za kuchimba Dhahabu na vifaa vinginevyo.
Kampeni hii ya kitaifa itakayofanyika katika mikoa yote Tanzania Bara kuanzia tarehe 18 Januari hadi 9 Aprili 9, 2026 imelenga kubadili fikra na mtazamo uliopo miongoni mwa watanzania kwamba uwekezaji ni kwa ajili ya raia wa kigeni na sio watanzania kwa kutoa elimu ya uwekezaji kwa makundi mbalimbali katika jamii na kujenga hamasa itakayosaidia kuchochea mwamko na kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa