Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.Martine Shigela ametoa wito kwa wananchi wote katika mkoa wa Geita kushiriki kikamilifu katima Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwezi Novemba 2024.
Mhe. Shigela ametoa wito huo alipokuwa akiongoza Kikao cha watumishi mbalimbali wa Serikali, Madiwani pamoja na Kamati za ulinzi na usalama za wilaya na Mkoa wa Geita kilichofanyika tarehe 18/09/2024 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Aloysius Geita Mjini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita ameeleza kuwa Serikali imejipanga vyema kuhakikisha wananchi Wanashiriki katika zoezi la Uandikishaji wapiga kura na kujitokeza kwa wingi siku ya Uchaguzi wa viongozi wetu wa Serikali za Mitaa siku ya tarehe 27 Novemba 2024.
‘’Serikali imepanga vituo vya kutosha kwa ajili ya kuwaandikisha wapiga kura, ambavyo vitakuwa jirani na makazi ya wananchi ili waweze kujiandikisha kiurahisi.’’Ameongeza Mhe.Shigela.
Mkuu wa Mkoa wa Geita pia amewaagiza waheshimiwa Madiwani na watendaji wa kata kuendelea na shughuli ya kuwaelimisha na kuhamasisha wananchi katika maeneo yao ili wananchi wote wafahamu umuhimu wa kushiriki katika zoezi la kuwachagua viongozi wao katika ngazi za mitaa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Ndugu.Mohamed Gombati ameeleza kuwa shughuli za usimamizi wa Uchaguzi huo zitasimamiwa na watakaoteuliwa kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi .
Kwa upande wake Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Geita Ndugu.Innocent Mabiki amesema uandikishaji wa wapiga kura utafanyika kwa siku kumi kuanzia tarehe 11-20 Oktoba na siku ya Uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa itakuwa tarehe 27 Novemba 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa