Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Ndugu Mohamed Gombati ametoa wito kwa wananchi wote wa Wilaya ya Chato na mkoa mzima kwa ujumla ambao wanasumbuliwa na matatizo ya mifupa, ubongo na mfumo wa fahamu kwenda kuwaona wataalam ili waweze kupatiwa matibabu .
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ametoa wito huo tarehe 6/11/2024 alipokuwa akizindua rasmi huduma za kibingwa na ubingwa bozezi za mifupa, ubongo na upasuaji wa mishipa ya fahamu ambazo zinatolewa na Madaktari kutoka Taasisi ya Mifupa na Ubongo (MOI) katika Hospitali ya rufaa ya Kanda Chato.
Ndg. Mohamed Gombati ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwajali wananchi wake na kutoa timu ya wataalam kwa lengo la kuja Mkoani Geita kutoa matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wote wanaosumbuliwa na matatizo ya mifupa, ubongo na mfumo wa fahamu.
“Serikali imetufanyia jambo kubwa sana ambalo limesogeza huduma hizo karibu na wananchi na kuwapunguzia gharama za usafiri, malazi na kero nyinginezo ambazo wangekumbana nazo wanaposafiri kwenda jijini Dar es Salaam kufuata huduma hizo. Hivyo ndugu wananchi wenzangu tumieni kikamilifu fursa hii adhimu ili kupata suluhisho ya matatizo ya kiafya yanayowasumbua”. Aliongeza Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI, Dkt. Bryson Mcharo ambaye ni Daktari bingwa na mbobezi wa mifupa amesema Serikali kupitia Taasisi ya MOI imekuwa na shauku ya kuhakikisha inawafikishia huduma za kibingwa kwa wananchi wa kanda ya ziwa ili kuwapunguzia umbali wa kusafiri na kusafirisha wagonjwa hadi Dar es Salaam hali iliyopelekea wakati mwingine kuwapoteza ndugu zao wakiwa njiani kufuata huduma hizo . Dkt. Mcharo ameongeza kuwa kwa wiki mbili watakazofanya huduma katika Hospitali ya kanda Chato wamelenga kuwahudumia wagonjwa 300.
Bi. Merina Wilson ni mkazi wa Wilaya ya Chato na mama anayemuuguza kijana wake ambaye alipata ajali na kuvunjika mguu ametoa shukrani kwa Madaktari bingwa waliotoka MOI ambao wamempatia kijana wake huduma ya kuwekewa vyuma na hali yake inaendelea kuimarika. Pia ameiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweka utaratibu wa kupeleka Madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa mbalimbali ambayo yanawasumbua wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa