Wananchi wa mkoa wa Geita wamehimizwa kutumia fursa iliyoletwa na Mahakama nchini Tanzania kwa jina “Mahakama Mtandano” ili kuweza kuwarahisishia upatikanaji wa huduma ya kimahakama lakini vilevile kuokoa muda mwingi uliokuwa ukitumika kwenda mahakamani badala yake sasa muda mwingi utumike kwenye shughuli za uzalishaji ili kujiletea maendeleo na hatimaye kufikia Tanzania ya Uchumi wa Juu.
Hayo yameelezwa leo Februari 2, 2022 wakati mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Rosemary Senyamule akitoa salamu zake kwa washiriki wa kilele cha wiki ya sheria nchini akiwa kama mgeni maalum ambapo kwa Geita imehitimishwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Geita, huku akipongeza utendaji wa Mahakam na kusisitiza mambo matatu kwa wananchi.
“kwanza nimpongeze Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof.Ibrahim Juma, watendaji wote wa mahakama kuanzia ngazi ya juu hadi chini kwa utendaji wao mzuri. Lakini pia nimpongeze Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiongoza nchi na kwa kuendelea kutoa fedha kwa ujenzi wa Mahakama. Niwaombe wananchi tutumie fursa hii ya Mahakama Mtandao ambayo huturahishia kufungua mashauri tukiwa mbali ili tutumie muda mwingi kujiletea maendeleo”, alisema Mhe.Senyamule.
Aidha mkuu wa mkoa huyo aliongeza kuwa, “bado kama mkoa tuna mambo matatu tunaendelea kuyasisitiza ambayo ni kuwahimiza wanafunzi kuacha utoro bila kusahau kuwa wazazi wenye watoto wenye umri wa kwenda shule ni lazima kuwaandikisha. Pia tuendelee kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19 kwa kupata chanjo, na tukumbuke wakati wa Sensa ya Watu na Makazi itakapofika basi tuwepo, tishiriki na tutoe taarifa sahihi ili kuiwezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo”
Mgeni rasmi wakati wa shughuli hiyo ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Geita Mhe.Cleofas Waane amesema “Mahakama ya Tanzania haijabaki nyuma wakati wa Mapinduzi ya nne ya viwanda na ndio maana inaenda kimtandao na kwamba kupitia Mahakama mtandao kumesaidia kurahisisha uendeshaji shughuli za kimahakama, kumepunguza msongamano wa wananchi mahakamani, kumeondoa woga kwa wananchi wanaoogopa majengo ya mahakama kupitia mahakama inayotembea, kumewezesha mawakili kupata rejea za hukumu na nyaraka mbalimbali. Vilevile Mahakama mtandao kupitia mfumo wa E-Wakili imewezesha kuwabaini mawakili vishoka ambao wamekuwa wakiharibu mwenendo wa kesi, hivyo tunajivunia”
Kwa upande wake Kaimu Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Geita Bi.Janeth Kisibo amesema Mahakama Mtandao imekuwa na faida lukuki na kutoa rai juu ya serikali kuboresha mtandao ili kuwezesha kupunguza msongamano wa mahabusu kwani kesi zitasikilizwa kwa wakati huku akiipongeza serikali kwa ujenzi wa mahakama ya Mbogwe na Nyang’hwale na kuwahimiza wananchi watambue kuwa haki inaendana na wajibu.
Akitoa salamu kwaniaba ya Mawakili wa Kujitegemea, Wakili Walta Karos ameeleza kuwa pamoja na uzuri wa Mahakama Mtandao kama kupunguza urasimu na kurahisisha uhuishaji wa leseni, changamoto bado ni kukatika kwa mtandao ambapo wameshauri itumike njia ya video wakati wa usikilizaji wa kesi, lakini pia kuhakikisha ulinzi wa taarifa na nyaraka na kuomba kesi zenye maslahi ya umma kurushwa mubashara mtandaoni.
Sherehe hizo ni kiashiria cha kuanza mwaka mpya wa kimahakama ambapo wiki ya sheria ilizinduliwa Januari 23, 2022 na kuhitimishwa Februari 2, 2022 kwa kutoa zawadi kwa washindi mbalimbali walioshiriki michezo wakati wa maadhimisho ya wiki hiyo.
Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa