Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa hamasa kwa wanawake wa Mkoa wa Geita kushiriki kwa wingi katika sekta ya madini kama njia ya kuwakwamua kiuchumi na kuchochea maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Gwajima ametoa hamasa hiyo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na hadhara ya wanawake waliojitokeza kwa wingi katika Kongamano la kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake ambayo kwa kanda ya ziwa yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ushirombo Wilayani Bukombe Mkoani Geita.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii amefafanua kuwa wanawake wengi wamekuwa wakijishughulisha baadhi ya kazi za usaidizi katika maeneo mbalimbali ya machimbo na wanachangia sehemu kubwa ya uchumi wa Nchi kupitia sekta ya madini hivyo imefika hatua ya wao kupata fursa sawa na wanaume kwa kupata umiliki wa maeneo ya uchimbaji ili kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa familia na jamii kwa ujumla.
“Serikali ya awamu ya sita imefungua dirisha la uwezeshaji wanawake kiuchumi kupitia mikopo inayotolewa hivyo napenda kutumia fursa hii kuwashauri wanawake wa Mkoa wa Geita kutumia mikopo inayotolewa na Serikali pamoja na Taasisi nyingine za kifedha kukuza Zaidi mitaji yao.” Aliongeza Mhe. Gwajima
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ametoa pongezi za dhati kwa Mhe. Gwajima kwa kuwasaidia wanawake kupata haki na heshima wanayostahili na kusimamia vyema majukumu ya jumuiya zote zinazofanya kazi kubwa ya kuwaunganisha wanawake wa Mkoa wa Geita. Pia ametoa ombi kwa Taasisi zote za kifedha kuendelea kupunguza riba za mikopo ili wanawake waweze kukopa bila hofu yoyote.
Kongamano la wanawake Kanda ya Ziwa lilibebwa na mada kuu isemayo ushiriki na nafasi ya mwanamke kwenye maendeleo ya Sekta ya Madini ikilenga kuhamasisha wanawake kushiriki Zaidi katika sekta hiyo hususan kwa kanda ya Ziwa ambapo Mkoa wa Geita una vikundi 43 vya wanawake vinavyomiliki leseni za uchimbaji madini na vikundi 20 kupatiwa vitalu vya uchimbaji madini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa