Na Boazi Mazigo-Geita
Ikiwa ni siku ya pili tangu kuwasili na kuanza kufanya kazi, Mkuu wa Mkoa Geita Mhe.MartinShigela amewataka Watumishi wa Umma kutoka Ofisi anayoiongoza kuhakikisha wanajipanga kuwahudumia wananchi kwakuwa tayari Serikali imewezesha mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
Ameyasema hayo Agosti 6, 2022 wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Nyumba ya Makazi ya Mkuu wa Mkoa kisha kumtaka Mshauri Elekezi ambaye ni Wakala wa Majengo nchini TBA kuhakikisha anamsimamia vyema Mkandarasi ili amalize kazi mapema iwezekanavyo kwa kuzingatia kwamba muda wa kukamilisha mradi umekwisha.
RC Shigela amesema, “kwanza nimefurahi kuona ujenzi unaendelea vizuri, niwapongeze viongozi waliotangulia kwa kazi nzuri. Pia nimshukuru sana Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini tena na kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za maendeleo ikiwemo utekekelezaji wa mradi huu unaogharimu fedha nyingi. Kikubwa ni watumishi wa umma kujipanga kuwahudumia wananchi kwani mazingira mazuri ya kufanyia kazi tunayo”
“niwapongeze TBA kwa usimamizi, lakini pia Mkandarasi kwa kuendelea na kazi, lakini ni muhimu kuhakikisha ujenzi huu unafikia mwisho, hakuna sababu ya kuchelesha mradi”. Ameongeza RC Shigela kisha kuwaalika wananchi kuja kupata huduma katika ofisi nzuri zilizopo eneo la Magogo mjini Geita akitoa rai kwa taasisi zinahozusika na Mawasiliano ya Simu, Maji na Barabara kuhakikisha maeneo ya Serikali yanapata huduma hizo stahiki.
Kwa upande wake QS. Glory Akyoo ambaye ni Mkadiriaji Majenzi kutoka TBA amesema, ujenzi ni wa Ghorofa 3 kwenye eneo la kilomita za mraba 6,112 kwa gharama ya Bilioni 6.5 hadi sasa Mkandarasi ametekeleza kazi kwa asilimia 90 na amelipwa kiasi cha shilingi Bilioni 4.4 hivyo kuahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kwamba kwa pamoja wataketi kikao cha pamoja ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kwani mkataba ulkuwa ni wa miezi 12 kuanzia Februari 26, 2020 hadi Februari 26, 2021 ambapo hadi sasa mkandarasi ameongezewa muda hadi mara tano hadi kufikia Julai 30, 2022.
Naye Mhandisi Makoye Luhya kwaniaba ya Mkandarasi Mayanga Construction Ltd amesema, anaishukuru Serikali kwakuwa imekuwa ikiwalipa na kwamba, kuchelewa kwa mradi ni kutokana na changamoto ya vifaa kuchelewa na kutoa ahadi yakuwa, kwakuwa kwa sasa vifaa vyote vipo eneo la kazi, atahakikisha hakuna sababu tena itakayopelekea kushindwa kukamilisha mradi kwa asilimia 10 zilizosalia.
Mwisho, Katibu Tawala Mkoa Geita Prof.Godius Kahyarara amempongeza RC Shigela kwa kutembelea mradi huo na kwamba maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa atayasimamia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa