Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita wamelezwa kutakiwa kujivunia mafanikio ya sekta ya Afya kwa kutembea kifua mbele huku wakitambua kuwa Wizara ya Afya inawathamini, inawajali na inawapenda, hivyo wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa mshikamano, umoja na upendo ili kukidhi matarajio ya wateja wao, wakiwemo wagonjwa ili kuhakikisha wanapata huduma iliyo bora katika eneo lao.
Hayo yameelezwa kwao na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalage Februari 23, 2022 alipokutana na kufanya kikao pamoja nao kwenye eneo la sehemu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa iliyopo mjini Geita akihimiza vilevile kuwa na lugha nzuri ya kuwajali wateja ili taswira nzuri iliyopo isije kuharibiwa.
“kwanza niwapongeze kwa kumpata Dkt. Japhet Simeo Mganga Mkuu Mkoa na Dkt. Mfaume Salum Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa utendaji wao na kuhakikisha hakuna mtumishi anadai madeni ya nyuma. Kama wizara mjue tunawathamini na ndiyo maana tumekuja kuongea nanyi. Lakini pia niwaombe mpendane, mshikamane na mshirikiane ili yote haya yakifanyika kwa pamoja tufikie matarajio ya mteja”. Alisema Dkt.Shekalage.
Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo aliwataka watumishi kutambua yakuwa hakuna asiye na thamani kwenye taasisi hiyo, kila mmoja ana thamani na ni wa muhimu na ndiyo maana hufanya kazi kwa kutegemeaana akitumia msemo wa kiiingereza usemao “nobody is useless, everyone is important”
Awali akiongea na watumishi hao, Mkurugenzi Msaidizi na Msimamizi wa Hospitali za Mikoa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Caroline Damian alisema, kwakuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya, basi itakuwa ni jambo jema ikiwa kila mmoja atahakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na matarajio ya wateja, na hivyo itakuwa ni kuwatendekea haki Wananchi, Wizara na Mhe.Rais kwaniaba ya Serikali bila kusahau matumizi sahihi ya mifumo iliyowekwa kukusanya mapato ili kupunguza utegemezi.
Akisoma taarifa, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Mfaume Salum alisema, pamoja na mafanikio waliyoyapata ikiwemo kulipa stahiki za watumishi na kutoa huduma bora, bado wanahitaji kuboresha miundombinu ya majengo ya zamani wanayoyatumia kwa kipindi hiki yaliyojengwa tangu mwaka 1956 ili kuwa na miundombinu bora zaidi bila kusahau kuiomba wizara kuongeza madaktari bingwa na gari la kubebea wagonjwa Ambulance.
Awali, Dkt. Shekalage alianza kutembelea maendeleo ya ujenzi wa majengo mbalimbali inapoendelea kujengwa hospitali mpya ya rufaa ya mkoa na kujionea shughuli ya uchimbaji msingi wa majengo ya wagonjwa mahututi (ICU), jengo la dharura (EMD) na eneo litakapojengwa jengo la mama na mtoto (Maternity Block).
Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima
Boaz Mazigo
Afisa Habari
Geita RS
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa