Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Profesa Riziki Shemdoe amewaasa watumishi wa umma katika Mkoa wa Geita kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuepukana na matokeo ya kurudisha nyuma kasi ya utekelezaji wa Miradi.
Profesa Shemdoe ametoa kauli hiyo hivi karibuni katika kikao na watendaji wa idara mbalimbali za Serikali na watumishi wengine wa umma katika ukumbi wa Nyerere ulioko viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Geita mjini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI amefafanua kuwa baadhi ya watumishi wamejenga desturi ya kutosimamia vyema miradi ya maendeleo na kupelekea miradi ya maendeleo kuzorota na kushindwa kutoa huduma kwa wananchi kwa muda uliokuwa umekusudiwa.
“Watendaji mnapaswa kufanya kazi kwa upendo na kutimiza wajibu wenu pasipo kusubiri ziara za viongozi wanaofika kukagua, msisubiri hadi mradi uharibike ndio mfike kutafuta suluhisho la changamoto zilizojitokeza wakati mlikuwa na muda wa kutosha kufuatilia kila hatua ya utekelezaji wake.” Aliongeza Profesa Shemdoe.
Sambamba na hayo Profesa Shemdoe ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya, Shule za msingi na sekondari pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja ambao umesimamiwa vyema na wataalam na kupata miradi inayoendana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Grace Kingalame ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuupatia Mkoa wa Geita fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inawanufaisha wananchi. Pia ameahidi kufanikisha utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na uongozi wa Mkoa utayafanyia kazi kwa maendeleo ya Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa