Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Ndugu Mohamed Gombati amewakumbusha watumishi wa umma kufanya kazi kwa upendo, umoja na ushirikiano pasipo kusahau kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa umma.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na watumishi wote wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita katika kikao kilichofanyika hivi karibuni kwenye Ukumbi wa mikutano katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Ndg. Mohamed Gombati amewasisitiza watumishi kutambua kuwa kila mmoja kulingana na kada yake ni mtu wa muhimu katika kuhakikisha shughuli za Serikali zinafanywa kikamilifu na kwa kuheshimiana pasipo kusahau viapo vyao vya kazi na urunzaji wa siri za ofisi kwa lengo la kuongeza umakini wa kazi pamoja na kuzisaidia Halmashauri kutimiza vyema majukumu yao.
Katika kikao hicho watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita walipata fursa ya kufanya zoezi la uchaguzi wa viongozi wapya wa timu ya michezo ya RAS Sports Geita ambao watakuwa madarakani ndani ya kipindi cha miaka minne kabla ya uchaguzi mwingine kufanyika.
Kikao cha watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kimefanyika kulingana na utaratibu wa kawaida ambapo agenda mbalimbali kuhusu utawala bora, kusikiliza taarifa kutoka Idara ya Utumishi, taarifa ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Mkoa, masuala ya utawala bora na mada kuhusu afya ya akili ziliwasilishwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa