WATUMISHI MKOA WA GEITA WATAKIWA KUTATUA KERO MBALIMBALI ZA WANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Geita Robert Gabriel Lughumbi amewataka watumishi na watendaji wa Mkoa wa Geita kufanya kazi kwa juhudi kubwa ili kuleta maendeleo kwa wananchi. Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi kati yake na Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga( Mkuu wa Mkoa Mstaafu) mheshimiwa Robert amesema kuwa wananchi wana matarajio makubwa sana na Serikali ya awamu tano hivyo ni lazima kufanya kazi kwa juhudi kubwa.
"Sikuja kulala nimekuja kufanya kazi lazima tuone mabadiliko ya haraka". Pia amewataka watumishi kutokutumia muda mwingi Ofisini bali waende field ili kuwasaidia wananchi kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula,biashara na kukuza biashara na mitaji ya wafanyabiashara.
Vile vile amewataka viongozi na watumishi kutokubali migogoro na kugawanywa lazima kuishi kwa upendo na umoja ili kufanikisha maendeleo Mkoani Geita kwa kuwa maendeleo ya Geita yataletwa na sisi wenyewe.
Mkuu wa Mkoa amemshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuwaletea wananchi wa Geita maendeleo kwa kipindi chote ambacho amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita. Kwa upande wake Ezekiel Kyunga Mkuu wa Mkoa Mstaafu amemweleza Mkuu mpya wa Mkoa kuwa wananchi wa Geita ni wachapakazi wanalima mashamba makubwa ili kujiletea maendeleo na wanashiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mheshimiwa Robert Gabriel Lughumbi anakuwa Mkuu wa Mkoa wa nne katika Mkoa wa Geita tangu Mkoa huu kuanzishwa mwaka 2012 akifuata watangulizi wake Magalula Said, Fatma Mwassa na Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Elias Kyunga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa