Mkuu wa Mkoa wa Geita Mheshimiwa Martine Shigela amewaasa waumini wa dini zote katika Mkoa wa Geita kuendeleza utamaduni wa kuthaminiana, kuheshimiana, kushirikiana na kupendana katika hali zote.
Mhe. Shigela ametoa ujumbe huo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na waumini wa dini ya kiislam pamoja na dini nyingine wakati wa Iftari maalum aliyoiandaa kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wake katika ukumbi wa Shule ya Sekondari St. Aloysius Geita mjini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita aliongeza kuwa mwaka 2025 umekuwa mwaka wa neema ya ajabu kwa sababu waumini wa dini zote kwa maana ya waislam na wakristo wamefunga kwa wakati mmoja, hivyo watu wote hawana budi kuzidi kuomba Amani, umoja na mshikamano vidumu katika Nchi yetu hususan katika mwaka huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Mhe. Shigela ametumia fursa hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwjaengea wananchi wake msingi wa Amani, upendo, utulivu na mshikamano pamaoja na kuendelea kuufungua mkoa wa Geita kimaendeleo kupitia ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi, ujenzi wa barabara za lami kuunganisha mikoa na kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Geita Nicholaus Kasendamila amepongeza jambo la imani lililofanywa na Mkuu wa Mkoa na kushauri jambo hilo liwe endelevu na la kuigwa kwa viongozi wote, pamoja na kuwakumbusha viongozi wa dini kuzidi kuwakumbuka katika dua na maombi yao viongozi wote wa Serikali katika kutimiza majukumu yao ya kila siku.
Wakitoa neno la shukrani, Viongozi wa Baraza la Waislam Mkoa wa Geita wametoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa namna anavyoshirikiana nao katika majukumu mbalimbali ya kiserikali pamoja na migogoro inayohitaji kufanyiwa usuluhishi bila ubaguzi wa aina yotote.
“ Mtu anayefanya mema ni lazima apongezwe, Mkoa wa Geita tuna bahati ya kumpata Mkuu wa Mkoa ambaye amewaunganisha viongozi wote wa Dini ambao wanaketi na kujadili masuala mbalimbali muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.” Waliongeza viongozi wa BAKWATA.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa