Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb) ameamsha ari ya wakazi wa Kijiji na Kata ya Nyamwilolelwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita pale alipozindua kwa kuwasha umeme uliotokana na utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa REA III sehemu ya kwanza akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, Mbunge wa Jimbo la Busanda, Mwenyekiti na Katibu wa CCM Wilaya ya Geita, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Meneja TANESCO Mkoa, Meneja Msaidizi Usambazaji na Huduma kwa Wateja kutoka Makao Makuu DSM na Meneja wa REA kanda ya ziwa alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi tarehe 17.08.2018 Kukagua, kufuatilia, na kutathmini utekelezaji wa kazi serikali iliyoitoa kwa mkandarasi inayotekelezwa mkoani Geita.
Mhe. Waziri Dkt. Kalemani amesema; anafikisha salamu zake kutoka kwa Mhe. Rais Magufuli anawasalimu sana wananchi wa Geita kwa ujumla. Pia Mhe Waziri amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata kwa wakazi wa Nyamwilolelwa, kwani shahuku waliyoionesha mbele yake juu ya umeme ni dalili inayotosha kuonesha kuwa wakazi wa Nyamwilolelwa wapo tayari kwa maendeleo kwakuwa umeme huu utatumika kwa uzalishaji na uanzishaji wa viwanda utaongezeka. Pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa geita kwa kuhamasisha maendeleo mkoani humo, lakini pia Mbunge wa jimbo hilo la Busanda kwa namna ambavyo amekuwa hachoki kuomba umeme kwa vijiji ambavyo havikuwa na umeme ndani ya jimbo lake.
Amesema “mhe. Mbunge, mara ya kwanza ulipata umeme kwa vijiji 20, mara ya pili vijiji 7, mara ya tatu mabayo ni hii umepata umeme kwenye vijiji 30 na vingine vitano kutokana na umeme utakaotoka Bulyanhulu Kahama kwenda Geita kwenye kituo kikubwa cha kupozea umeme (Sub Station) kitakachojengwa mapema mwezi Agosti, 2018; hivyo utakua umebaki na vijiji 32 kati ya 89, nakupongeza sana”. Aliongeza kwa kusema, “nimekuja Geita pia kufuatilia na kukagua taasisi za umma ambazo hazina umeme kama shule, zahanati n.k. kwa maana kazi ya serikali ni kusogeza miundombinu karibu na wananchi ila kazi ya kuingiza umeme ndani ya taasisi ni ya Halmashauri, hivyo nawaagiza wakurugenzi na wenyeviti wa Halmashauri kuhakikisha mnatenga bajeti ili taasisi hizo zipate umeme. Nitaomba kupata orodha kutoka kila taaisi ambayo haijafikiwa na umeme”. Mhe.Dkt. Kalemani aliwaambia wananchi wa Kijiji hicho kuwa, mkandarasi ahakikishe anafikisha umeme kwenye Kata hiyo kwanza, ikiisha ndiyo ahamie pengine na kusisitiza asiruke kijiji.
Mhe. Dkt. Kalemani amesema, ikumbukwe kuwa bei ya kuunganishiwa umeme huo ni shilingi elfu ishirini na saba (Tshs.27, 000/=) na mtu yeyote asithubutu kuwaibia wananchi lakini pia alimtambulisha mkandarasi ili wananchi waepuke vishoka.
Pamoja na kupewa umeme kwa vijiji hivyo, Waziri Dkt. Kalemani alitoa vifaa vyenye jina UMETA (yaani Umeme Tayari) 250 kwa wateja 250 watakaolipia mapema kwa wale ambao hawajaweka mfumo wa umeme (wiring) kwenye nyumba zao ili waanze kuutumia kwa vyumba vinne kwa niaba ya serikali lakini yeye pia ametoa vifaa hivyo kumi (10) kama mchango wake. Pia amemwagiza mkandarasi kuweka umeme kwenye gereza ka Butundwe ili kurahisisha huduma na kumsisitiza kuwa anatakiwa amalize kazi kwa wakati kwani hataongezewa mwezi, siku wala saa katika utekelezaji wa mradi. Kisha kwenda kuwasha umeme kama ishara ya uzinduzi.
Akishukuru kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhadisi Gabriel amesema, “ hakika naipogeza serikali hii ya awamu ya tano chini ya Mhe. Rais Magufuli, na Mhe. Waziri tufikishie salamu zetu kwake. Lakini pia ninahaidi tutailinda miundombinu hii ili isiweze kuharibiwa na wasio na mapenzi mema ya ukuaji wa uchumi wetu. Pia Mhandisi Gabriel aliendelea kusisitiza kuwekwa umeme kwenye taasisi za Umma kama mashule na zahanati; lakini pia wiki ijayo nitakuja tuchimbe msingi wa zahanati kwa kuwa Geita hakuna kulala mpaka kieleweke kwani azma ya Mkoa ni ifikapo mwaka 2019 kabla ya uchaguzi Geita iwe na zahanati kila kijiji lakini mwisho akamuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri kuchangia mifuko ya saruji tayari kuifanikisha shughuli hiyo”.
Mbunge wa jimbo la Busanda Mhe. Lolensia Bukwimba, amemshukuru Mhe. Waziri kwa upendo ambao serikali iliyouonesha kwa wananchi. Pia ameshukuru ombi la kupelekewa umeme Chankorongo ili maji yapatikane kwa nguvu ya umeme.
Mwisho mwenyekiti wa CCM Wilaya Mhe.Barnabas Muhoja Mapande alishukuru kwa kusema “jambo ulilolifanya Mhe. Waziri halijawahi kutokea, huu ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM wa kasi inayotakiwa na hakika wananchi wamehamasika sana na pongezi kwa Mhe. Rais Magufuli utufikishie. Lakini bila kusahau, tunashukuru kwa RC wa Geita kwa kuwa ni mchapakazi, anatekeleza kwa vitendo ni kiongozi bora”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa