Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo (Mb), ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinatumia mbinu zozote kisheria kuhakikisha fedha ya Serikali zilizopotea zinarudishwa, alipokutana na kuongea na Baraza la Madiwani,Wananchi na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 05.09.2018.
Ni baada ya kupotea kwa zaidi ya shilingi Bilioni 2 za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya Elimu, Afya, Maji na Utawala ambayo haijatekelezwa na fedha kutojulikana zilipo.
Mhe. Jafo amesema, “nimekuja mwenyewe hapa, lakini hata kama sijaenda saiti, lakini mwenendo wa Halmashauri hii hauniridhishi wa asilimia 100, kwani hata nilipokuwa Naibu Waziri, nilikuja hapa na tukakaa katika ukumbi huu na nikaahidi kutafuta fedha mjenge ofisi, lakini zimeliwa" na kumpongeza Mkurugenzi mteuliwa mpya Bi. Mariam Chaulembo kwa kazi ambayo ameifanya hadi sasa na kusema angependa kupata wakurugenzi wengi kama yeye.
Amewasihi watumishi wa umma kutozichezea fedha za Serikali na kwamba yeye kama Waziri mwenye dhamana anaona kufanya mchezo huo ni sawa na mtu kuyachezea maisha yake ya baadaye (future life).
Katika hatua nyingine, Mhe Jaffo ameagizwa kukamatwa kwa watumishi wa umma saba wanaotuhumiwa kuhusika na ubadhilifu mkubwa wa fedha za umma na mmoja kwa masuala ya watumishi hewa wakiwemo ;
1. Bw. Carlos Gwamagobe (aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
2. Bw. Donatus Pangani (Mweka Hazina)
3. Bw. Godson Mbelwa (Mhasibu)
4. Gudala Kija (Afisa Kilimo)
5. Bw. Robert Machimu mtoa fedha (Cashier)
6. Bw. Alfred Joseph (Katibu wa Afya) na
7. Bw. Paul Zahoro (Afisa Habari)
Na kisha baada ya uchunguzi kukamilika, watakaokutwa na makosa basi taratibu zifuatwe za kuwakisha kwenye vyombo vya sheria.
Wa nane aliyeagiza kushikiliwa na jeshi la polisi ni Bw. Muhando Bakari Muhando (Afisa Utumishi) Kwa tuhuma za kuhusika na watumishi hewa.
Mhe. Waziri amevitaka vyombo vya uchunguzi kuhakikisha vinaenda mbele zaidi katika uchunguzi wake na kwamba hata kama itagundulika walioshiriki kusababisha upotevu wa fedha hizo wamestaafu, kufukuzwa kazi, ama kuhama, waitwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao ikiwemo kufilisiwa ama kutaifishwa kwa mali zao kwa mujibu wa sheria kulingana na yaliyotendeka akiongeza kwa kusema “hata kama ni viongozi wa siasa wakikutwa wameshiriki nao washughulikiwe”.
Mhe. Jafo hakuishia hapo, bali pia amesikitishwa na kitendo cha madiwani kulifumbia macho suala hilo chini ya uongozi wao na akasema ni muda muafaka wa viongozi hao kujitathmini pamoja na kuyaagiza Mabaraza yote ya Madiwani nchi nzima kuhakikisha kamati za fedha zinapata taarifa ya kibenk (bank statement) kabla ya kujadili masuala yahusuyo mapato na matumizi, lakini pia Wakuu Wote wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa.
Mwisho Mhe. Waziri aliwataka watumishi wengine kufanya kazi kwa uadilifu na kutokukubali kushiriki vitendo vya ubadhilifu wa mali za umma kwani itakua ni kuwataabisha wananchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ameeleza kusikitishwa na tabia hiyo yenye kuchafua jina la mkoa na kusema kuwa anaahidi kutekeleza yote yaliyoelekezwa akisaidiana na timu yake, akisema atasimamia uchunguzi ufanyike tena wa kina ili kupata majibu ya suala hilo na yeyote atakayebainika atachukuliwa sheria.
Fedha ambazo zimepotea zinahusisha miradi ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R), Ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Mradi wa Maji na Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Afya (Wodi, Maabara na Nyumba za Kuhifadhia Maiti (Mortuary).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa