Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe (MB), ametembelea na kuona miradi mbalimbali inayotekelezwa Mkoani Geita akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Shaaban Ntarambe, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Mhandisi Deusdedith Kakoko, pamoja na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Geita Mhandisi Harun Senkuku.
Miradi aliyoitembelea ni pamoja na Bandari ya Nyamirembe iliyoko kijiji na Kata ya Nyamirembe Wilayani Chato ambayo ilikua ikitumika tangu enzi ya Mkoloni ambayo kwa sasa haifanyi kazi. Mhe. Waziri amewaeleza wananchi wajiandae kufurahi kwani muda si mrefu bandari hiyo itafufuliwa na kuanza kazi; ni baada ya kujitokeza kumlaki kwa fuaraha baada ya kumuona akitembea kwenye bandari hiyo.
Amesema “mwezi wa nane mwaka huu tunasaini mkataba, tunairudisha Bandari ya Nyamirembe. Na sasa tunajenga meli kubwa, itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria elfu moja mia mbili (1,200), mizigo tani mia nne (400) ambayo itapita hapa kwenda Bukoba ndiyo maana kituo hiki lazima tukijenge na mkandarasi anaingia hapa mwezi wa nane. Hivyo ni ushindwe mwenyewe mwananchi kwa sababu sasa meli itakuwepo, barabara ya lami ipo, kiwanja cha ndege kinaendelea kujengwa unataka nini tena?” alimaliza kwa kushangiliwa na wananchi.
Kisha, Mhe. Waziri amembelea na kujionea maendeleo ya hatua ya ujenzi wa barabara ya Bwanga – Biharamulo yenye urefu wa kilomita sitini na saba (Km.67) inayojengwa kwa kiwango cha lami na kufurahishwa na hatua iliyofikiwa baada ya kupewa taarifa kuwa, barabara hiyo imeshajengwa hadi kilomita hamsini na saba (Km.57) hivyo bado kilometa kumi (Km.10) ili iweze kukamilika.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Gabriel amemshukuru Mhe. Waziri kwa ujio wake lakini pia kwa kuteuliwa kuwa msimamizi wa wizara hiyo na kupendekeza maombi ya kutanuliwa barabara za kuingia Geita mjini ili ziwe mbili wakati wa kuingia na mbili wakati wa kutoka, lengo ikiwa ni kupunguza ajali na kuokoa maisha ya watumia barabara waendesha baiskeli na watembea kwa miguu ambao hupata ajali kutokana na msongamano barabarani. Mkuu wa Mkoa pia ametumia nafasi hiyo kuomba Daraja la Wavuka kwa Miguu (Pedestrian Bridge) karibu na soko jipya la kisasa Mjini Geita litakalokuwa na duka lenye bidhaa zinazotengenezwa Tanzania pekee katika kutafuta soko la bidhaa za ndani , jambo lililopelekea Mhe. Waziri kusema amelipokea ombi hilo na kuahidi kulishughulikia kwa kumuagiza Meneja TANROADS Mkoa kuandaa maombi hayo na kumwasilishia ili aweze kusaidia utekelezaji wake. Kisha alimshukuru Mhe. Waziri kwaniaba ya wananchi wa Geita kuendelea kufungua milango ya fursa na kutoa wito kuhusiana na jukwaa la fursa za biashara litakalofanyika mkoani Geita kuanzia tarehe 15 hadi 16.08.2018 na kwamba endapo bandari hiyo itakamilika, uwanja wa ndege ukakamilika, basi wageni wengi watakuja kwani kuna vivutio vya utalii lakini pia biashara ya dhahabu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Shaaban Ntarambe alimhakikishia Mhe. Waziri kuwa, wananchi wapo tayari kupokea maendeleo na ameshukuru kwa namna ambavyo mkandarasi anayejenga barabara hiyo ana mahusiano mazuri na wananchi wa Chato jambo linalosaidia utekelezaji mzuri wa mradi usiwe na migogoro.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa