Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ametoa agizo kwa Mgodi wa Dhahabu Geita( GGML) kuketi na Wakurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa lengo la kuandaa na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya CSR kuanzia mwaka 2018 hadi 2021.
Mhe. Mavunde ametoa agizo hilo tarehe 14 Aprili 2025 wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa Miradi ya Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni ya GGM kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Wizara ya Madini jijini Dodoma.
Waziri wa Madini ameeleza kuwa ameitisha kikao hicho kwa lengo la kutafuta njia bora ya kutekeleza miradi ya CSR, kutatua changamoto zilizopo na kuhakikisha wananchi wa Geita wananufaika na rasilimali madini yanayochimbwa katika maeneo yao.
“Wananchi wa Geita wanatamani kuona matokeo ya moja kwa moja ya uwepo wa mgodi huo kwa kupitia miradi ya maendeleo, hivyo kuna umuhimu wa kukamilisha utekelezaji wa miradi ya nyuma kuanzia mwaka 2018-2021 ili kuwezesha uanzishwaji wa miradi mipya yenye tija kwa jamii.” Aliongeza Mhe. Mavunde
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela amehimiza ushirikiano wa karibu baina ya GGML na Serikali kwa kuwasisitiza GGML kuhakikisha miradi iliyosainiwa inatekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa makubaliano ili wananchi wa Geita waweze kunufaika.
Wakichangia maoni Wabunge wa majimbo ya Geita mjini, Geita Vijijini na Busanda wameitaka kampuni ya GGML kuhakikisha inakamilisha miradi ya CSR kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu utakaoendana na gharama zilizotumika ili wananchi wa Geita wayaone matunda ya uwepo wa Mgodi huo.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Anglo Gold Ashanti Ndg. Simon Shayo amesema kwamba Kampuni ya GGML iko tayari kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Geita ili kuhakikisha wananchi wa Geita wananufaika na miradi ya CSR ambayo kwa sasa kiasi cha Shilingi Bilioni 21 imetekwa kwa ajili ya utekelezaji na ukamilishaji wa miradi ya kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2024 ambayo ilikuwa imekwama kwa sababu ya changamoto mbalimbali.
Kikao hicho kimehusisha viongozi kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Uongozi wa Mkoa wa Geita, Wabunge wa Wilaya ya Geita pamoja na wawakilishi wa GGML kwa nia ya kupata muafaka kuhusu changamoto za utekelezaji wa miradi ya CSR na kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wananchi wa Geita wananufaika na uwepo wa Mgodi huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa