Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa mgeni rasmi amefunga maonesho ya kwanza na ya Kihistoria ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini ya Dhahabu katika Uwanja wa CCM Kalangalala uliyopo Mjini Geita tarehe 30.09.2018.
Mhe. Majaliwa ameanza kwa kutoa salam za Mhe. Rais Magufuli kwa wananchi wa Mkoa wa Geita akiwaambia kuwa, Mhe. Rais amefurahishwa sana na tukio hilo muhimu na kisha kupongeza juhudi za Mkoa, TanTrade, TCCIA Geita, GEREMA, na Wizara na kusema amefurahishwa na namna ambavyo washiriki walivyojitoa kutumia rasilimali za nchi ipasavyo kwa maendeleo yao ya kiuchumi na Taifa letu kwa ujumla lakini pia kuishukuru kamati ya maandalizi pamoja na taasisi zilizoshiriki na kuziachia benki changamoto ya kuanzisha vitengo vya kupokea dhahabu ili kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo.
Amesema, “mabenki anzisheni utaratibu wa kuweka madini ya wananchi yakiwemo dhahabu, ili huyu mwananchi badala ya kwenda kulaliwa kwenye minada aende benki ahifadhi ili hata mwakani achukue yakiwa yameongezeka thamani. Hivyo natoa wito kwa mabenki, mbadilikeni, Mkurugenzi Mkuu Benki kuu kaeni na Benki zenu za Biashara anzeni utaratibu wa kupokea dhahabu”.
Waziri Majaliwa pia akawapa habari njema Mkoa wa Geita kuwa, Serikali imetenga dola za kimarekani milioni 500 kwa miji 25, Geita ikiwemo. Hivyo kwa Mji wa Geita zimetengwa jumla ya dola za kimarekani milioni 45 kutoka chanzo za Ziwa Victoria. Pia akasisitiza juu ya Wanaume kupenda kupima UKIMWI na kutotegemea wanawake kupima kisha kutumia majibu yanayopatikana ili kutafsiri afya zao.
Kwa upande wake Mhe. Angellah Kairuki (Mb), Waziri wa Madini, ameonesha kusikitishwa kwa Wizara anayoisimamia kutokana na kadhia kwa wananchi wenye nyumba zaidi ya mia nane za wakazi wa Nyamalembo na Katoma zilizopasuka kutokana na mitetemo inayotokana na shughuli za Mgodi wa GGM licha ya Taasisi ya Serikali ya GST kufanya tathmini na kutoa matokeo yaliyothibitisha pasipo shaka kuwapo kwa madhara kutokana na shughuli za Mgodi, hivyo akatoa siku chache kutoka sasa kufikia tarehe 24.10.2018 wananchi waathirika wawe wameanza kulipwa fidia.
Naye Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita akatoa msimamo wa Serikali ya Mkoa wa kuhakikisha Geita inabadilika kulingana na Rasilimali zilizopo. Ameeleza pia kutofurahishwa na wenye nia ovu ya kuirudisha nyuma Geita na kusema yeye kwa sasa anajifananisha na gari la wagonjwa (Ambulance) akisema atawasomba wagonjwa wote (wananchi wenye matatizo kwenye sekta ya madini) na kuwaelekeza kwa daktari (wataalamu wa madini) ili wapate suluhu ya changamoto.
Mwisho, maonesho yalihitimishwa kwa kutoa zawadi kwa mgeni rasmi pamoja na washindi mbalimbali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa