Ni kauli ya mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya maonesho ya pili ya Nanenane Kanda ya ziwa magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera, maonesho yaliyohudhuriwa na zaidi ya washiriki 300 katika eneo la Nyamhongolo, Manispaa ya Ilelemela Jijini Mwanza yaliyodumu kwa wiki moja tangu Agosti Mosi hadi Agosti Nane 2019.
Akiongea wakati wa kuahirisha maonesho hayo, RC Mongella amewataka wananchi na washiriki wa maonesho hayo kuhakikisha wanakwenda kutumia elimu waliyoipata katika kuboresha shughuli zao za kilimo, mifugo na uvuvi katika kuifikia Tanzania ya viwanda huku akipongeza kuimarika kwa maonesho hayo na kuwapongeza Simiyu kwa kuwa mwenyeji maonesho ya Nanenane Kitaifa.
“nawapongeza waoneshaji wote wenye mabanda na watoa huduma. Na kama malengo ya maonesho haya yalivyo, ya kutoa elimu na uelewa kama alivyotangulia kusema RC Geita Eng.Robert Gabriel, ni jambo la muhimu sana kwani mahali pengine ni gharama kubwa kupata huduma hizi. Hivyo tuishukuru Serikali yetu kwa kuweka mwongozo huu wa kuwa na maonesho ambayo watu mbalimbali wakiwemo binafsi na mashirika ya umma hutoa uelewa kwa wananchi kwani ni kwaajili yao na kipekee tuyatumie kushiriki kujenga uchumi wetu”, alisema Mongella.
RC Mongella ameendelea kusema, kwa muda mfupi aliopita kwenye mabanda hayo ameelimika sana na kushuhudia mambo makubwa hali iliyopelekea yeye na RC Gabriel kukubaliana maonesho hayo yaendelee hadi siku ya jumapili kwani kiu ya wananchi bado ni kubwa ya kuendelea kujifunza.
Kabla ya kutangaza siku ya kufungwa rasmi maonesho hayo, RC Mongella alisema, kama kanda wameamua kuwa na maonesho zaidi ya hayo ya nanenane hivyo kutumia fursa hiyo kuwaalika washiriki na wanachi wote kuhamia kwenye Maonesho ya Pili ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yatakayofanyika Mjini Geita kuanzia tarehe 20-29/09/2019, kisha kukabidhi zawadi kwa washindi mbalimbali Nyang’hwale iking’ara kwa mkoa wa geita kwa kunyakuwa tuzo za kundi la ufugaji na halmashauri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Eng.Robert Gabriel amesema anategemea kuona wengi wamebadilika kutokana na kuona kwao maonesho hayo na kwa kuona wamekuwa wapya akisema kwaniaba ya mkoa wa geita anaamini kuwa, mafanikio ya wanamwanza ni sawa na ya wanageita, hivyo akatumia fursa hiyo kuwaalika kushiriki maonesho ya pili ya teknolojia na uwekezaji kwenye sekta ya madini yatakayofanyika Geita.
RC Gabriel amesema, “halmashauri ni vyema sasa mkatumia ujuzi huu mkawape vikundi vya akinamama, vijana na wenye ulemavu wanaopokea mkopo wa masharti nafuu ili waweze kuzalisha kisasa na wainuke”
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Christopher Kadio amemshukuru mgeni rasmi kwa kutembelea mabanda na kujionea shughuli mbalimbali kutoka kwa waoneshaji na kutoa maelekezo na ushauri kwa wadau hao huku akitoa ushauri wa kutumia teknolojia ya vitendea kazi vya kisasa na kuachana na kilimo cha kutumia jembe la mkono, walau watumie Plau, jembe la kukokota na Ng’ombe na kwamba maonesho hayo yanaenda kwa dhana ya uchumi wa viwanda ambayo inalenga katika kuongeza thamani ya mazao. Hivyobasi, kufanya hivyo itakuwa ni uungaji mkono kauli ya Mhe.Rais iliyojikita kufikia uchumi wa kati mwaka 2025.
Mwenyekiti wa kamati ndogo ya tathimini ya maonesho ya kilimo, na sherehe za wakulima nanenane kanda ya ziwa magharibi Mwl.Jovitha Mwombeki amesema makundi 16 yalishindanishwa ambapo washindi wa kwanza hadi wa tatu walipata vikombe, fedha taslim na vyeti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa