Kampuni ya ACACIA kupitia Mgodi wake wa Dhahabu wa Bulyanhulu umetiliana saini makubaliano kuchangia ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati 32 ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale tarehe 05.08.2018 ikiwa ni katika kutekeleza Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, na marekebisho yake ya mwaka 2017, Kifungu cha 105, kinachoagiza wamiliki wa leseni za madini kutekeleza miradi ya maendeleo katika jamii inayowazunguka yaani wajibu wa makampuni ya madini katika jamii (CSR).
Akiongea baada ya utiaji saini makubaliano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel ameupongeza uongozi wa mgodi kwa kutekeleza takwa la kisheria kwa kutoa kiasi cha fedha milioni mia tano zitakazokamilisha maboma 32 yaliyojengwa kwa jitihada za wananchi na kusema kwa sasa ni vijiji vinne tu ndivyo havijaanza ujenzi kutokana na kuwa na changamoto ya kuwa na eneo la kujenga zahanati hizo bila mgogoro, ambapo amesema ndani ya miezi mitatu anaamini maeneo hayo yatakuwa yamepatikana na ujenzi kuanza mara moja na ni imani yake kuwa kufikia mwezi wa tano mwaka 2019, mkoa utakua unafungua zahanati ya mwisho kila kijiji. Amesema tuwatumikie wananchi na angependa usimamizi uwe mzuri ili baada ya miezi mitatu Zahanati hizo zifunguliwe.
Amesema, “nawapongeza Bulyanhulu kwa uamuzi wa kutoa fedha hizi kwa ajili ya kukamilisha Zahanati kila kijiji ikiwa ni utekelezai wa Ilani ya Chama Tawala CCM na uungaji juhudi za Mhe. Rais”. Pia amewataka viongozi wa Wilaya na Halmashauri kuhakikisha wanasimamia vyema ukamilishaji wa miundombinu hiyo na kuwa hatomvumilia yeyote atakayejaribu kuchezea fedha yoyote ya utekelezaji miradi ya maendeleo.
Mhe. Mhandisi Gabriel amewapongeza viongozi wa vijiji ambavyo vimekuwa na jitihada za kujenga Zahanati na kumwagiza Mkurugenzi kuwachukulia hatua viongozi walio chini yake watakaoshindwa kuwahamasisha wananchi kushiriki maendeleo yani viongozi wenye matokeo hasi na siyo chanya. Pia amewashauri kuja na mpango wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya ili kuendana na kasi hiyo ya Zahanati kila kijiji.
Mkuu wa Mkoa akataumia fursa hiyo kukemea na kuonya juu ya ubadhilifu uliyofanyika kwenye Halmashauri hiyo wa zaidi ya Shilingi Bilioni 2 ambazo hazionekani zilipo na kuwaambia kuwa hatosalia yeyote aliyehusika na kwamba atafuatilia kwa nguvu zake zote na uchunguzi utawahusu wote wanaohusishwa hata kama ni wastaafu au wamehama kituo cha kazi, na kuwaagiza Halmashauri kukusanya mapato ili iweze kujiendesha vizuri na kutokukubali kupokea mapato yasiyo halali bali kupata mapato stahiki.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na Buzwagi Bw. Benedict Buzunzu amesema, anaamini makubaliano hayo yataleta mapinduzi katika eneo la afya kwa Halmashauri ya Nyang’hwale akisema, “mapema mwaka huu, Nyang’hwale walitushirikisha mipango yake ikiwemo hii kampeni ya Zahanati kila kijiji nasi tukaona ni vyema nguvu yetu tuipeleke huko". “Hivyo kampuni ya ACACIA kupitia Mgodi wa Bulyanhulu tutaelekeza fedha hii itoe vifaa vikakamilishe Zahanati hizo 32 na ni furaha yetu kuwa sehemu ya mafanikio haya na huu ni mwanzo tu ado tutaendelea kushiriki na tunaushukuru uongozi wa Wilaya kwa ushirikiano ambao umekuwepo, alimaliza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Bi. Mariam Chaulembo akawashukuru Bulyanhulu kwa kuja wenyewe bila kulazimishwa na yeyote, lakini pia akaushukuru uongozi wa mkoa kupitia kamati ya ulinzi na usalama na akiahidi kusimamia utekelezaji wa ukamilishaji wa Zahanati hizo ili wananchi wapate huduma stahiki na kwa wakati.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Hamim Gwiyama aliwaeleza waliohudhulia hafla hiyo kuwa anaamini kwamba kampeni ya Mkuu wa Mkoa sasa inatimia kutokana na kampuni hiyo kutoa fedha hizo.
Halmashauri ya Nyang’hwale ina jumla ya vijiji 62, ambapo vijiji 14 vina zahanati, Vijiji 13 Zahanati hatua za ujenzi zinaendelea, Vijiji 3 ndiyo wanashulikia upatikanaji wa maeneo na Vijiji 32 ndiyo vipo katika hatua za ukamilishaji ambapo fedha hizo zimeelekezwa.
Hafla hiyo ilihudhuliwa pia na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Denis Bandisa, watumishi ofisi ya Mkuu wa Wilaya na waandishi wa habari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa